DAR-Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ameeleza kuwa Wizara hiyo inaandaa utaratibu wa kulipeleka Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC katika viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam 2025 (Sabasaba) ili wananchi wapate fursa ya kuliona.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa tarehe 29 Juni, 2025 ametoa taarifa ya Serikali kupitia mkutano na Waandishi wa Habari katika Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara; Sabasaba, Dar es Salaam ambapo amezungumzia masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali katika kuwaletea Watanzania maendeleo.
Amesema hatua hiyo itawawezesha wananchi wengi zaidi kuliona pia kukutana na wachezaji wa Klabu ya Yanga ambayo ilitwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara 2025 katika uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 25, 2025.
Msigwa ameyasema hayo Juni 29, 2025 jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea masuala mbalimbali yanayoendelea katika Maonesho ya Kimataifa ya 49 ya Biashara ya Dar es Salaam 2025 yaliyoanza Juni 28, 2025.
Amesema,katika maonesho ya mwaka huu wananchi watakaohudhuria watapata fursa ya kuwaona wanamichezo maarufu wa Tanzania pia kupata burudani na michezo mbalimbali itakayokuwa ikioneshwa katika banda la Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo ambalo kwa mwaka huu limepewa jina la Kijiji cha Sanaa.
“Katika maonesho ya mwaka huu, tumewaletea burudani ndani ya kijiji chetu ambayo itahusisha muziki wa aina zote yaani Bongo Fleva, Singeli, Hip hop, Taarabu na ngoma za asili). Shughuli hii itakua ikifanyika kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 6:00 usiku ambapo wasanii mbalimbali watapanda jukwaani kutumbuiza,” amesema Msigwa akitoa wito kwa kwa wananchi kutembelea banda la maonesho la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.