DAR-Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imeandaa Tamasha la Sabasaba ambalo ni bidhaa mpya ya Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwa mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 29, 2025 Jijini Dar es Salaam, Msigwa amesema tamasha hilo linafanyika kwa mara ya Kwanza mwaka huu ambapo TANTRADE imetenga eneo kubwa la zaidi ya ekari moja ambalo litatumika kwa ajili ya Tamasha hilo lililoanza Juni 28, 2025 na litakwenda mpaka mwisho wa Maonesho ya Sabasaba Julai 13, 2025.
Amesema,ndani ya tamasha hilo kutakuwa na burudani ya muziki waaina zote ukihusisha Singeli, Dansi, Bongoflava na Taarabu kila siku kuanzia mchana mpaka usiku.
Pia kuna maonesho ya taasisi za Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambazo zinatoa huduma za papo kwa papo zikiwemo za kusajili wasanii, utoaji wa vitambulisho vya waandishi wa habari (Press Card), usajili wa magazeti na huduma kuhusu mikopo ya wasanii kupitia mfuko wa Utamaduni na Sanaa.
“Wizara tumewakaribisha wadau mbalimbali kuja kutangaza huduma zao, tuna huduma za vyakula vya asili na vya kawaida, nyama choma, na vinginevyo. Pia wasanii wetu maarufu wa filamu na muziki pia wameweka mabanda yao kwa ajili ya kuonesha kazi zao," ameeleza Msigwa.
Ameongeza kuwa katika eneo hilo kutakuwa na huduma ya usajili wa kidijitali wa vyama na mashirikisho ya michezo kupiitia mfumo wa SARS, utoaji wa vibali vya kupiga picha za filamu kwa raia wa kigeni na wazawa, usajili wa kazi za sanaa na ubunifu, usajili na utoaji wa vitambulisho na leseni kwa wasanii.
Aidha, Msigwa ameeleza kuwa katika tamasha hilo, Wizara imewapatia mabanda ya maonesho baadhi ya wasanii na wadau wa kazi za ubunifu waliojitokeza ili waweze kuonesha na kuuza huduma na kazi zao kwa washabiki wao wakiwemo Kombolela, Jacquiline Wolper, Gambo Zigamba, Punchline, Studio 19, Lady Jaydee, Alikiba - Crown Media, African Princess (Nandy), Chido Salon na Anna Collection.
“Katika tamasha hili wananchi watapata nafasi ya kuwaona wasanii, kuwauliza maswali na kununua bidhaa za wasanii kwenye kijiji chetu. Pia katika tamasha letu la Sabasaba tutakua na maonesho ya mavazi kutoka kwa wanamitindo mbalimbali maarufu hapa nchini akiwepo Anna Collection,”amesisitiza.
Mbali na wasanii hao na watu maarufu, Msigwa amesema katika tamasha hilo kutakuwa pia michezo ya watoto ili kuwezesha watoto hususani wanafunzi walio likizo kupata burudani ya michezo mbalimbali katika kijiji cha burudani akiwaomba wazazi na walezi wawalete watoto wao kucheza katika eneo hilo.
