NA LWAGA MWAMBANDE
MACHI 8,2025 mechi ya Yanga SC dhidi ya Simba SC maarufu kama Kariakoo Derby ambayo ilipangwa kupigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam iliahirishwa kutokana na mgogoro ulioibuka kabla ya mchezo huo.
Miongoni mwa sababu za kuahirishwa kwa mechi hiyo,Simba SC walidai kuwa walizuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.Ni licha ya wao kuwa ni timu ya ugenini na kulingana na Kanuni ya 17(45) ya Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya ugenini inapaswa kuruhusiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi kabla ya siku ya mchezo.
Aidha,Simba walidai kuwa walizuiwa kufanya mazoezi na walikosa haki yao ya kisheria, jambo lililosababisha wao kutangaza kutoshiriki mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Ingawa nao Yanga SC walisisitiza kuwa, mchezo bado unafanyika kama ilivyopangwa, na walikanusha madai ya Simba SC kuhusu kuzuiwa kufanya mazoezi uwanjani hapo.
Kutokana na changamoto hiyo, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilichunguza madai ya tukio hilo na kuamua kuahirisha mchezo ili kutoa nafasi ya uchunguzi zaidi, bodi baadaye ilipanga upya ratiba na kuazimia mtanange huo utapigwa Juni 15,2025 katika uwanja ule ule.
Uamuzi huo haukuwaridhidha,Yanga SC hivyo wamekataa kushiriki mchezo huo, wakidai kuwa hawatashiriki kwa sababu ya mgogoro uliotokea awali.
Kwa Simba SC wanasisitiza kuwa,wanajiandaa kwa ajili ya mchezo huo na wanatarajia kushinda ikiwa ni ushindi muhimu kuelekea Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Licha ya maswali mengi aliyonayo mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande hoja yake inaendelea kusalia kwamba bado hatima na ustawi wa soka la Tanzania ipo mikononi mwa waliopewa jukumu la kusimamia,hivyo ni wajibu wao kuamua kuhusu wimbo wa Hatuchezi. Endelea;
1. Liwe jua iwe mvua, hatuchezi,
Ndivyo tulivyochagua, hatuchezi,
Hakuna wa kutangua, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
2. Tulifanya kosa sisi, hatuchezi,
Walifanya wao hasi, hatuchezi,
Polepole mwendokasi, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
3. Mashindano si chandimu, hatuchezi,
Hili suala muhimu, hatuchezi,
Hakuna ubinadamu, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
4. Kwanza mechi mpinzani, hatuchezi,
Ni kweli sio utani, hatuchezi,
Tunatema mate chini, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
5. FA fainali, hatuchezi,
Madai yetu kamili, hatuchezi,
Tulipwe kikwelikweli, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
6. Kweli huu ni mchezo, hatuchezi,
Japo hatuna uwezo, hatuchezi,
Twaendeleza makwazo, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
7. Ni mtego maamuzi, hatuchezi,
Kuamua hiyo kazi, hatuchezi,
Hapo nani mtetezi, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
8. Mpira wa Tanzania, hatuchezi,
Ndiyo tunaisikia, hatuchezi,
Ni kujisikitikia, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
9. Kama hili la mashiko, hatuchezi,
Basi tulipe mwaliko, hatuchezi,
Kwetu uwe ni mkoko, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
10. Kama ni la hovyohovyo, hatuchezi,
Kwamba ni mpango hovyo, hatuchezi,
Tuwaache hivyohivyo, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
11. Yanachoka masikio, hatuchezi,
Kimeshakua kilio, hatuchezi,
Kuna hapana na ndio, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
12. Tufikiri ya maana, hatuchezi,
Kuchekacheka hakuna, hatuchezi,
Makali waweze ona, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
13. Tuendako tutafika, hatuchezi,
Kama hiyo yainuka, hatuchezi,
Watu wanaadhirika, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
14. Tunautaka ubingwa, hatuchezi,
Hatuwezi tukafungwa, hatuchezi,
Tunao wetu walengwa, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
15. Kusema si kazi ngumu, hatuchezi,
Madhara yake magumu, hatuchezi,
Yaondoa utimamu, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
16. Bora tukomeshe hii, hatuchezi,
Kanuni zote tutii, hatuchezi,
Isiwepo nchi hii, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
17. Kesho isijetokea, hatuchezi,
Na muda ukapotea, hatuchezi,
Mijadala kukolea, hatuchezi,
Ndio wimbo unatamba, hatuchezi.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602