Rais Dkt.Mwinyi afarijika kwa ongezeko la Mahujaji, ahimiza umoja na amani nchini

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameonesha kufarijika zaidi kutokana na idadi ya Mahujaji wa Zanzibar wanaokwenda Hijja kuongezeka huku akiendelea kusisitiza amani,umoja na mshikamano kwa wananchi katika kuyafikia maendeleo endelevu nchini.
Mheshimiwa Rais Alhaj Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Juni 7,2025 alipojumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu na wananchi katika Baraza la Eid Al Adha katika Ukumbi wa Dkt.Ali Mohammed Shein uliopo Tunguu, Zanzibar.

"Hakika sikukuu hii ni neema yetu nyingine kutoka kwa Mola wetu mlezi baada ya Waislamu wenzetu kwa mamilioni kutoka mataifa mbalimbali duniani kukamilisha ibada ya Hijja katika Mji mtakatifu wa Makka.
"Tunamuomba Mwenyezi Mungu mtukufu azikubali Hijja na ibada zote walizozifanya Mahujaji katika miji mitakatifu ya Makka na Madina na awarudishe nyumbani kwa salama."

Pia, Rais Dkt.Mwinyi ameshukuru na kupongeza jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kuelimisha na kuhamasisha Waislamu mbalimbali wenye uwezo nchini kwenda kutekeleza ibada ya Hijja ikiwa ni miongoni mwa nguzo muhimu za Uislamu.

"Hakika,inatia moyo kuona kila mwaka idadi ya ya wananchi wanaotoka Zanzibar kwenda kutekeleza ibada ya Hijja ikiongezeka."

Mheshimiwa Rais amesema, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar (UTAHIZA) imeonesha kuwa, Mahujaji 2,460 kutoka Zanzibar wamekwenda kutekeleza ibada ya Hijja kupitia taasisi za Zanzibar mwaka huu.
Kutokana na juhudi za pamoja zinazofanywa na Serikali kupitia Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na taasisi zinazosafirisha Mahujaji nchni, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, katika kuzifanyia kazi changamoto zilizokuwepo pamoja na uhamasishaji kwa ujumla ana matumaini makubwa kuwa idadi ya Mahujaji wa Zanzibar itazidi kuongezeka kila mwaka.

Vilevile,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amewashukuru wote waliofanikisha safari za Mahujaji wa Zanzibar kwa kuwapatia huduma mbalimbali, hivyo kuweza kufanikisha safari zao za kwenda kutekeleza ibada ya Hijja.

"Shukurani maalum ninazitoa kwa Serikali ya Saudia Arabia kwa ushirikiano walioutoa pamoja na kukubali shirika lao la ndege kuanza safari za moja kwa moja kutoka Zanzibar hadi Saudi Arabia, hivyo kuondokana na usumbufu waliokuwa wanaupata Mahujaji wa Zanzibar kabla ya kuanza safari za moja kwa moja."
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa,ili kuhakikisha watu wengi zaidi kutoka Zanzibar wanakuwa na uwezo wa kwenda kutekeleza ibada ya Hijja, Serikali kupitia Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana itaongeza kasi katika kuhakikisha dhamira ya kuanzisha Mfuko wa Hijja nchini inafikiwa kwa haraka.

Amesema, ibada ya Hijja ambayo tunaadhimisha kumalizika kwake kama zilivyo ibada nyingine huwa na mafunzo ya kuzingatiwa katika kukuza imani zetu na ucha Mungu ili tuweze kufanikiwa katika maisha yetu ya duniani na kesho mbele ya haki.
"Moja katika mafunzo ya kuzingatia katika ibada ya Hijja ni kudhibiti kwa kauli ya Mwenyenzi Mungu iliyosisitizwa na Mtume Muhammad S.A.W juu ya umoja na undugu wa Waislamu.

"Umoja unaoonekana katika siku za Hijja ni mafunzo muhimu kwetu wanadamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni msingi muhimu wa kuondokana na ubaguzi wa aina zote na kuishi kwa amani na mshikamano."
Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa,umoja na mshikamano una umuhimu mkubwa katika nchi yetu katika kudumisha amani tuliyo nayo ili tuweze kupata mafanikio zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news