ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inaendelea na mkakati wa kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika maeneo mbalimbali nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akifuatilia matangazo ya moja kwa moja kupitia ZBC ya uwasilishaji wa Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2025/2026, inayowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Mhe. Saada Mkuya Salum, katika Baraza la Wawakilishi tarehe 12 Juni 2025.Akiwasilisha Mwelekeo wa Hali ya Uchumi mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri wa Nchi, Fedha na Mipango,Dkt. Saada Mkuya Salum katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar amesema, Serikali imepanga miradi ya kimkakati kwa kuzingatia faida zitakazopatikana.
Vilevile na yenye kuleta matokeo ya haraka katika kuimarisha shughuli za kiuchumi na kuinua hali za wananchi.Dkt. Saada amesema, mikakati hiyo ni katika maeneo ya uzalishaji, kugharamia utoaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji,umeme,kuimarisha utalii na uwekezaji kwa lengo la kuinua kipato cha mwananchi, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Aidha,Waziri Saada ameeleza kuwa, mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa Miaka Mitano 2021-2026, imeigawa miradi hiyo katika kutumia fursa za Uchumi wa Buluu, mazingira wezeshi na uimarishaji wa miundombinu, kuimarisha mageuzi ya kiuchumi, kukuza rasilimali watu na huduma za kijamii pamoja na kuimarisha utawala na uhimilivu.
Akizungumzia suala ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, Waziri huyo amesema Uchumi wa Zanzibar unakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 7.3 mwaka 2025 kutoka wastani wa asilimia 7.1 mwaka 2024.
Amesema,uingiaji wa watalii watakaotembelea nchini unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 12.6 kutoka watalii 736,755 kwa mwaka 2024 hadi watalii 829,929 mwaka 2025.
Aidha amefahamisha kuwa, Serikali inaendelea kutekeleza kwa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara za mjini na vijijini, ujenzi wa uwanja wa Ndege Pemba, bandari ya Mangapwani na ukarabati wa Bandari ya Malindi.
Akizungumzia kuhusu mfumuko wa bei, Dkt. Saada ameeleza Serikali inaendelea na hatua za kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei ili kubakia katika tarakimu moja pamoja na kuongezeka kwa uhamasishaji wa ukusanyaji wa mapato.
Pia,usimamizi wa matumizi ya Serikali pamoja na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza thamani na miradi ya uwekezaji kwa Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akiwasilisha hotuba ya Kamati bajeti ya Baraza la Wawakishi kuhusu majumuisho ya Mijadala ya Bajeti za Wizara kwa mwaka wa Fedha 2025/2026 Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mwanaasha Khamis Juma ameiomba Serikali kuhakikisha kuwa tathmini ya fidia kwa wananchi walioathiriwa na miradi inakamilishwa haraka.
Sambamba na malipo ya fidia hizo yatolewe kwa wakati ili kuondoa malalamiko ya wananchi na kuruhusu utekelezaji wa mradi kuendelea kwa ufanisi.
Aidha,amefahamisha kuwa kukamilika kwa zoezi hilo kutaendelea kuimarisha uhusiano mwema kati ya Serikali na wananchi.Waziri Saada amewaomba wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupokea na kujadili Mwelekeo wa Hali ya Uchumi wa Zanzibar kwa Mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2025/2026 wenye kugharimu kiasi cha shilingi trilioni 4.54.








