NA GODFREY NNKO
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi wanazozifanya katika kuliongoza taifa.
Sambamba na kuimarisha huduma za ustawi wa jamii na maendeleo ya watoto na vijana kwa maslahi ya taifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Khatib Mwadin Khatib wakati akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Mheshimiwa Anna Athanas Paul.
Ni katika hafla iliyofanyika Juni 9,2025 jijini Dar es Salaam wakati Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana Tanzania (VACS-2024).
"Pia,shukrani ziende kwa Ofisi za Taifa za Takwimu (NBS na OCGS), pamoja na wadau wakiwemo Shirika la Kimataifa la Kimarekani la Centers for Disease Control and Prevention (CDC) Tanzania, UNICEF na Tanzania Health Promotion.
"Walioshirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Zanzibar pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum- Tanzania Bara kwa mchango wao mkubwa wa kifedha na kitaalamu katika kufanikisha utafiti wa kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana 2024 na hatimaye leo tunatangaza matokeo ya utafiti huu."
Bw.Khatib amesema,kwa kutambua madhara yanayotokana na tatizo la ukatili, na kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa kwanza wa ukatili dhidi ya Watoto na Vijana 2009, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikiendelea kufanya jitihada mbalimbali za kupambana na ukatili dhidi ya watoto na vijana.
Pia, amesema Serikali imekuwa ikiandaa na kutekeleza Sheria ya Watoto namba 6 ya 2011, kuandaa na kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto 2017-2022.
Vilevile kutekeleza programu ya Familia Bora Taifa Imara, kuanzishwa na kuimarishwa kwa madawati ya Polisi ya Jinsia na Watoto, Vituo vya Mkono kwa Mkono na huduma za Ustawi wa jamii.
Aidha,kuimarisha huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, kuendelea kuhamasisha jamii na familia kuhusiana na malezi bora na uwajibikaji kwa watoto, kuelimisha watoto na wanafunzi katika skuli na madrassa.
Lengo la kufanya hivyo, Bw.Khatib anesema ni ili kujikinga na kuripoti matukio ya ukatili na udhalilishaji kupitia vyombo vya sheria na huduma ya simu kwa mtoto kwa kutumia namba 116.
"Ukatili dhidi ya watoto na vijana ni tatizo linalohitaji juhudi za makusudi ili kulitokomeza kwa mashirikiano baina ya Serikali, asasi za kiraia,wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla.
"Baada ya kutangazwa kwa matokeo haya, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Zanzibar itaendelea kufanya mapitio na marekebisho mbalimbali ya sheria, sera na mipango ili kuboresha na kutekeleza afua mbalimbali za kuwalinda Watoto na Vijana dhidi ya ukatili katika jamii zetu."
Akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana Tanzania (VACS-2024), Waziri Dkt.Gwajima amesema,matukio ya ukatili dhidi ya watoto na vijana nchini yamepungua.
Amesema,utafiti huu ulilenga kupima kiwango cha ukatili wa kingono, kimwili na kihisia dhidi ya watoto na vijana wa kike na wa kiume nchini Tanzania na kuelewa hatari na athari za kiafya zinazohusiana na ukatili huu.
"Utafiti huu ulifanyika kati ya mwezi Machi na Juni, 2024 na uliwafikia zaidi ya watoto 11,414 wenye umri wa miaka 13 hadi 24 kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar."
Amesema,kwa mujibu wa utafiti huo ambao umefanywa na watafiti wabobezi unaonesha kuwa, matukio ya ukatili wa kingono kwa watoto wa kike yamepunua kutoka asilimia 33 hadi 11.Pia,matukio ya ukatili dhidi ya watoto wa kike yamepungua kutoka asilimia 76 hadi 24 huku ukatili wa kihisia matukio ya kikatili yamepungua kutoka asilimia 25 hadi 22.
Kwa upande wa watoto wa kike,Mheshimiwa Waziri Dkt.Gwajima amesema kuwa, matukio ya ukatili upande wa kingono yamepungua kutoka asilimia 21 hadi tano,kimwili kutoka asilimia 74 hadi 21.
Waziri Dkt.Gwajima ameongeza kuwa, kwa upande wa ukatili wa kihisia kwa watoto wa kiume matukio yamepungua kutoka asilimia 31 hadi 16.Utafiti huo ni wa pili kufanyika ndani ya miaka 15 tangu ule wa kwanza wa Kitaifa kufanyika mwaka 2009 nchini.








