Tanzania yaonesha ufanisi katika kulinda watoto dhidi ya ukatili,utafiti wathibitisha

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Juni 9,2025 imetangaza matokeo ya utafiti wa Kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana (Violence Against Children and Youth Survey-VACS2024) wa mwaka 2024.
Matokeo hayo yameonesha maendeleo na mafanikio makubwa ambayo Tanzania imepiga katika kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kingono,kimwili na kihisia.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ambaye ametangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari,wadau mbalimbali kutoka serikalini, sekta binafsi ndani na nje ya nchi amesema, hiyo ni ishara njema kwa Taifa na jamii kwa ujumla.
"Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana, 2024, Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika kupunguza ukatili dhidi ya watoto na vijana.

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (Tanzania Bara) na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Zanzibar) zimesimamia na kuongoza utafiti huu wa kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana, 2024."

Waziri Dkt.Gwajima amesema ni kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), Wizara ya Afya (MoH - NASHCoP), Ofisi ya Rais TAMISEMI, taasisi za ZIHHTLP na NPHL.

"Utafiti huu ulilenga kupima kiwango cha ukatili wa kingono, kimwili na kihisia dhidi ya watoto na vijana wa kike na wa kiume nchini Tanzania na kuelewa hatari na athari za kiafya zinazohusiana na ukatili huu.

"Utafiti huu ulifanyika kati ya mwezi Machi na Juni, 2024 na uliwafikia zaidi ya Watoto 11,414 wenye umri wa miaka 13 hadi 24 kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar."
Amesema,tafiti za kitaifa kama hizi ukiwemo utafiti wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto na vijana wa mwaka 2024 ni za ubora wa hali ya juu katika kuweza kupima viwango na aina mbalimbali za ukatili, na kuweka msingi wa mipango ya ulinzi na usalama wa watoto na vijana.

Vilevile amesema,suala la ukatili dhidi ya watoto na vijana ni la ukiukaji wa haki za binadamu na pia linaleta changamoto kubwa za afya katika jamii na kubadilisha maisha ya watu wanaopitia ukatili.

Waziri Dkt.Gwajima anasisitiza kuwa,ukatili huleta athari za muda mrefu za kiafya ikiwa ni pamoja na matatizo ya afya akili, mawazo ya kujiua, tabia hatarishi za ngono.

Athari nyingine amesema ni uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya zinaa ikiwemo VVU, matumizi ya dawa za kulevya.
Pia, amesema ukatili hupunguza fursa mbalimbali za kimaendeleo na kuongeza umaskini katika jamii.

"Huu ni utafiti wa pili wa kitaifa, ambao umefanyika baada ya miaka 15 tangu utafiti ule wa kwanza wa mwaka 2009. Napenda kuwapa habari njema kuwa, matokeo ya utafiti yanaonesha ukatili umeshuka kwa kiwango kikubwa ukilinganisha utafiti wa 2009 na huu wa 2024."

Amesema, utafiti wa kwanza wa mwaka 2009 ulionesha kuwepo kwa ukatili wa kingono, kimwili na kihisia miongoni mwa watoto na vijana.

Kupitia matokeo aliyoyatoa ya utafiti huu wa pili,Dkt.Gwajima amesema kuwa,kwatoto wa kike ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 33 hadi asilimia 11.
Pia,ukatili wa kimwili umepungua kutoka asilimia 76 hadi asilimia 24 na ukatili wa kihisia umepungua kutoka asilimia 25 hadi asilimia 22.

Vilevile kwa watoto wa kiume, Waziri Dkt.Gwajima amesema kuwa,ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 21 hadi asilimia tano.

Aidha,ukatili wa kimwili umepungua kutoka asilimia 74 hadi asilimia 21 na ukatili wa kihisia umepungua kutoka asilimia 31 hadi asilimia 16.

"Matokeo haya ya utafiti huu yatawezesha Serikali na Wadau kuboresha na kuandaa mipango,programu na mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukatili nchini itayoimarisha ulinzi na usalama wa watoto na vijana na maslahi mapana ya kizazi cha sasa na cha baadae."
Mbali na hayo,Waziri Dkt.Gwajima amesema, pamoja na mwenendo huu wa kupungua ukatili, bado Serikali itaendelea kuongeza nguvu zaidi katika kuzuia na kupinga vitendo vya ukatili viunavyojitokeza katika jamii.

Amesema, kupungua kwa vitendo vya ukatili huu inaonesha mafanikio makubwa yaliyotokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wadau katika kupinga na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto na vijana, kwa kuendelea kutoa elimu mbalimbali kwa umma, pamoja na juhudi za wizara.

Ni kuendelea kuimarisha mifumo ya kisheria kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mtoto Sura ya 13 ili kuondoa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wake na kuimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto.
Kutekeleza na kuratibu Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA wa Awamu ya Kwanza 2017/182021/22 na Awamu ya Pili 2023/242029/30) ambao unalenga kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili.

Waziri Dkt.Gwajima amesema, pia Serikali inatekeleza Programu ya Kitaifa ya Tanzania ya Kizazi Chenye Usawa (2021/2022) (2025/2026) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa.

Jambo lingine ni kutoa huduma kwa manusura wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kwa kushirikiana na wizara za kisekta na wadau mbalimbali.

Aidha,kuratibu na kusimamia Kampeni ya Taifa ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni (Child Online Protection-COP) katika mikoa ya Tanzania Bara.

Waziri Dkt.Gwajima amesma,kampeni hiyo inalenga kuwaelimisha wazazi, walezi, na watoto kuhusu usalama wa mtoto anapotumia mitandao.
Pia,kuratibu afua za kijamii kwa kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza vitendo vya ukatili, kuwezesha wanawake kiuchumi na upatikanaji wa haki, ulinzi, na malezi chanya ya watoto.

"Na kuokoa watoto wanaoshi na kufanya kazi mtaani kwa kuratibu juhudi za kuwaokoa watoto walioko katika mazingira hatarishi mitaani na kuwapatia huduma stahiki."

Waziri huyo amesema,Serikali pia inaratibu na kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika nyanja zote za maendeleo.

Ameongeza kuwa, Serikali inaratibu utoaji wa mafunzo kuhusu Sayansi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa Maafisa kutoka mikoa na halmashauri zote za Tanzania Bara.
Lengo la kufanya hivyo ni ili kuimarisha usimamizi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM 2021/22 - 2025/26).

Amesema, pia wizara inatoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka kila mkoa ili kuwawezesha kutoa taarifa sahihi kuhusu MMMAM na kuelimisha jamii.

"Tunatoa pia huduma katika vituo 32 vya Mkono kwa Mkono (One Stop Centers) na kushughulikia mashauri ya watoto kwa kutumia mfumo wa usimamizi wa mashauri ya watoto (NICMS 2017)."

Waziri Dkt.Gwajima ameendelea kufafanua kuwa,Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum itafanya tathmini, mapitio na maboresho ya Sera na Sheria zilizopo.
Sambamba na uimarishaji wa programu za kisekta za kuzuia na kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya makundi yote kwa kufanya uchambuzi wa afua zilizoainishwa katika MTAKUWWA wa Pili na kulinganisha na matokeo ya utafiti huu wa pili.

Amesema,hatua hii itasaidia katika kuongeza bajeti na rasilimali watu ili kuzuia ukatili dhidi ya makundi yote na kuboresha huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili.

"Hivyo nitoe rai kwa wadau wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha tunaimarisha ulinzi na usalama wa watoto na vijana kwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyotokea katika jamii zetu pamoja na kuendelea kutoa elimu kupitia vyombo vyetu vya habari."
Hata hivyo, Waziri Dkt.Gwajima amesema, suala la ukatili katika jamii linahitaji ushirikiano baina ya Serikali kupitia wizara za kisekta,asasi za kiraia na jamii ili kuhakikisha watoto wote wanalindwa,kusaidiwa na kuwezeshwa kufikia ndoto zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news