DODOMA-Katibu Mkuu Wizara ya Madini,Mhandisi Yahya Samamba amesema hadi kufikia tarehe ya leo Juni 28, 2025 Sekta ya Madini imekusanya Maduhuli ya kiasi cha shilingi Trilioni 1.063 ikiwa imebaki siku moja tu kukamilisha Mwaka wa Fedha 2024/25.

Ameyasema hayo leo Juni 28, 2025 wakati akifunga Bonanza la Wizara ya Madini lililowakutanisha pamoja watumishi wa Wizara na taasisi ambapo wameshiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete, riadha, kuvuta kamba, mchezo wa kukimbia na magunia ambapo timu na watumishi walioshinda katika michezo hiyo wamepatiwa medali na vikombe.
Mwaka wa Fedha 2024/25 Sekta ya Madini ilipangiwa kukusanya shilingi trilioni 1 ambazo zimeingizwa Mfuko Mkuu wa Serikali.

"Tumeweza kukusanya trilioni 1 na point bila kuwepo mgodi mpya. Hakuna mwaka huko nyuma tuliosogelea shilingi 900 bilioni lakini mwaka huu tumeweza kukusanya kiasi hicho hii ikiwa ni sawa na wastani wa kukusanya shilingi bilioni 84 kila mwezi," amesema Mhandisi Samamba.
Ameongeza kwamba, kufuatia mwenendo mzuri wa makusanyo katika Sekta ya Madini nchini, katika Mwaka wa Fedha 2025/26, Wizara imepangiwa kukusanya Shilingi Trilioni 1.2 na hivyo, kuwataka watumishi kuongeza bidii ili Sekta ya Madini iwe moja ya taasisi ambazo zitaongeza mapato ya ndani ya nchi yatakayoiwezesha nchi kujitegemea na kueleza, "Mhe. Rais amesema tuongeze makusanyo ya ndani kuiwezesha nchi kujitegemea."

"Unapokuwa GST, TEITI, Tume ya Madini, TGC au Wizarani usijione siyo sehemu ya Wizara," amesema Mhandisi Samamba.
Katika hatua nyingine, amepongeza hatua ya Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanza kununua dhahabu kama akiba ya taifa na kusema suala hilo si dogo ililinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo shughuli za uchimbaji zilikuwa zikifanyika pasipokuwepo akiba ya dhahabu.

Pia, ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha watumishi kujitokeza na kushiriki zoezi la kupiga kura wakati wa uchaguzi.
Mwisho amemtaka Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kuweka utaratibu wa kuwa na mabonanza yasiyopungua mannne Kwa mwaka kuendelea kujenga umoja na mshikamano baina ya watumishi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Tume ya Madini,Dkt.Janeth Lekashingo akizungumza katika bonanza hilo amewataka watumishi kuendelea kujenga mahusiano na mawasiliano miongoni mwao huku akisititiza kujenga tabia ya kufanya mazoezi.
Naye, Katibu Mtendaji Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhan Lwamo amesema afya njema inasaidia kuongeza tija ya kazi na hivyo kuwahamasisha waendelee kufanya mazoezi.