NA GODFREY NNKO
TUME ya TEHAMA nchini (ICTC) inatarajia kuratibu Jukwaa la Tanzania la Akili Unde (Tanzania Artificial Intelligence Forum) ikiwa ni jukwaa la kwanza la kihistoria nchini.
Jukwaa hilo ambalo ni jumuishi kwa watu wote linatarajiwa kufanyika Julai 28 hadi 29,2025 jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo Juni 20,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dkt.Nkundwe Mwasaga wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya tume yaliyopo Upanga jijini Dar es Salaam.
"Wengi wenu mmeona maendeleo na mapinduzi yanayoletwa na Akili Unde (AI) ambapo inapata coverages kubwa sana, na nchi nyingi zinaangalia namna gani ya kuweza kuzitumia hizi teknolojia hasa Teknolojia ya Akili Unde katika kuleta maendeleo ya kijamii,kiuchumi kwa namna mbalimbali.
"Na sisi hapa Tanzania, teknolojia hizi tumeanza kuzitumia, wote tunafahamu vizuri."
Amesema,Mahakama ya Tanzania katika miaka miwili iliyopita tayari imeshaanza kutumia Akili Unde, pia inaendea kutumika shuleni,vyuoni, afya na sekta mbalimbali.
"Sasa kutokana na hicho, wizara yetu ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kupitia Tume ya TEHAMA tuliona ni wakati muafaka tuanzishe jukwaa la Tanzania la Akili Unde (Tanzania Artificial Intelligence Forum) kwa hiyo hili litakuwa jukwaa la kwanza ambalo litafanyika mwezi wa saba,mwaka huu 2025 tarehe 28 na 29 jijini Dar es Salaam."
Amesema,jukwaa hilo litawakutanisha watu mbalimbali. "Akili Unde tofauti na teknolojia nyingi za habari zilizopita inamgusa kila Mtanzania.
"Inawagusa watumiaji au walaji wa Akili Unde,inawagusa wabunifu, inawagusa wanafunzi, wafanyakazi wa Serikali, watu wa sekta binafsi, wakulima.
"Kwa ujumla Akili Unde inaleta mapinduzi makubwa katika teknolojia," amesema Dkt.Mwasaga huku akifafanua kuwa ni mapinduzi makubwa kwa sababu ni mara ya kwanza katika historia ya mabadiliko ya kiteknolojia ambapo vitu vinavyotengenezwa na binadamu, vinakuwa vina uwezo wa kuweza kufikiri na kufanya maamuzi yanayofanana (si kama binadamu) na binadamu.
"Kwa hiyo,katika maendeleo ya teknolojia duniani tumefikia hatua kwamba, kitu ambacho zamani tulikuwa tunafikiria mtaalamu anaandika programu, lakini programu inafanya kama kile kilichoandikwa,sasa hivi tumefikia kwamba, vitu vinaweza kupata taarifa vikafikiri vyenyewe na vikatoa maamuzi yake.
"Kwa hiyo hayo ni mabadiliko makubwa sana na hayo mabadiliko yanahitaji jukwaa, jukwaa ambalo tutakutana watu wote,tutajadili mambo mbalimbali."
Amesema, jukwaa hilo litaongozwa na kauli mbiu ya "Tunatengeneza Kesho ya Tanzania ambayo Itakuwa inatumia Akili Unde inayofuata Maadili yetu, Masuala ya Utawala wa Taarifa ili kuleta Maendeleo jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii."
Amesema,katika jukwaa hilo si tu kwamba watajadili Akili Unde bali wataangazia maadili ya Tanzania.
Amesema, Akili Unde yenyewe inahitaji taarifa,hivyo masuala ya taarifa kupitia kongamano hilo watayaangazia kwa kina.
"Sababu ya kutengeneza kaulimbiu hii ni kwa sababu, imeonekana wazi wale ambao wameendelea vizuri katika Akili Unde, utakuta ndiyo nchi ambazo zina taarifa nyingi."
Ameeleza kuwa,hali halisi iliyopo duniani ni kwamba taarifa za nchi nyingi zinatunzwa katika nchi kubwa mbili duniani iliwemo Marekani na China.
"Kwa hiyo,wenye taarifa ndiyo wanaweza kufanya shughuli zao zikawa shindanishi zaidi, kwa hiyo na sisi tunataka tuangalie namna gani, na Serikali imeshaanza kufanya hatua nyingi za kutengeneza vituo vya taarifa (kanzidata hapa Tanzania),"amesisitiza.
Pia, amesema Serikali imetunga sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi ambayo inataka taarifa zetu zikae hapa nchini.
"Kwa hiyo tutaangalia kwa mawanda yake,tutaangalia masuala ya Akili Unde, tutangalia pia masuala ya utawala wa taarifa ili vyote hivyo tuhakikishe kwamba vinafanya vitu vikubwa viwili, kuleta maendeleo ya kijamii, maendeleo ya kiuchumi lakini jumuishi. Hatutaki mtu aachwe katika Mapinduzi haya."
Vilevile amesema, katika jukwaa hilo wataangalia Akili Unde ambazo zipo katika maendeleo ya kisasa zaidi ambapo wataangazia bunifu zinazofanywa na Watanzania.
Tags
Akili Unde (AI)
Artificial Intelligence
Habari
Tume ya TEHAMA
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari




