MANYARA-Julai 25,2025 Mahakama ya Wilaya ya Babati katika shauri la uhujumu uchumi Na. 15921/2025 imemtia hatiani mshtakiwa aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Zahanati ya Endagaw mkoani Manyara,Bw.Mohamed Twalib Baya kwa kosa la kughushi kinyume na kifungu cha 333,335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya 2022
(Mfano wa sahihi.Picha na Mtandao).
Mshitakiwa alighushi sahihi za watia saini katika akaunti ya Zahanati ya Endagaw na kuchukua fedha jumla ya shilingi 8,015,000 ambazo alizifanyia ubadhirifu.
Akisoma hukumu hiyo,Mheshimiwa Victor Kimario,Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Babati, amemtia hatiani mshtakiwa baada ya mshtakiwa huyo kufanya makubaliano (plea bargaining) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hapo awali mshitakiwa alishtakiwa kwa kufanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha shilingi 8,015,000 kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 kama ilivyorejewa mwaka 2022 pamoja na kuisababishia Mamlaka hasara kinyume na Aya 10(1) katika jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa [Sura ya 200 Marejeo ya 2022].
Pia,alishtakiwa kwa makosa ya kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335 (a) na 337 vya sheria ya kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya 2022.
Mshtakiwa amepewa adhabu ya kulipa faini ya kiasi cha shilingi 200,000 au akishindwa kutumikia kifungo cha gerezani kwa muda wa mwaka mmoja pamoja kurejesha fedha alizozifanyia ubadhilifu kiasi cha shilingi 8,0150,000 kwa muhanga.
Hadi hukumu inasomwa mshtakiwa amerejesha kiasi cha shilingi 4,000,000 katika akaunti ya Zahanati ya Endangwe (Muhanga) iliyopo Bank ya NMB na kiasi kilichobaki atakirejesha kabla au ndani ya mwezi mmoja.
Shauri hilo lilikuwa linaendeshwa na waendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Manyara ambao ni Neema Gembe, Davis Masambu na Catherine Ngessy.
.jpeg)