DODOMA-Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu leo Julai 17, 2025 ameshiriki uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uliofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC).
Uzinduzi huo umefanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ametoa wito kwa Watanzania wote kushiriki katika utekelezaji wa Dira hiyo ili kufikia lengo kuu la kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi, la haki na linalojitegemea.
Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 kulingana na Serikali ni kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi jumuishi unaopunguza umasikini, unaozalisha ajira na kuchochea mauzo ya nje ya bidhaa, kuongeza tija katika uzalishaji sambamba na uongezaji wa thamani kwenye mifugo, madini, misitu pamoja na kilimo.
