ARUSHA-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuvutia washiriki wa Kongamano la Wenyeviti wa Bodi na Wakurugenzi wa Taasisi za Umma linaloendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha.

Miongoni mwa viongozi waliotembelea banda la NHC ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bi. Joyce Mapunjo, ambapo alipata fursa ya kujionea huduma, mafanikio na fursa mbalimbali zinazotolewa na Shirika.
Kongamano hilo, ambalo linatarajiwa kufunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, limewaleta pamoja viongozi wa mashirika ya umma, wenyeviti wa bodi na watunga sera kwa lengo la kujadili mbinu za kuimarisha taasisi za umma na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Kupitia ushiriki wake, NHC inaendelea kuonesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za kimkakati, sambamba na kuongeza ubunifu, ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
