BoT yaendelea kuwapa elimu wananchi Maonesho ya Nanenane 2025

DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma kuanzia tarehe 01 hadi 08 Agosti 2025.
Kupitia ushiriki wake, Benki Kuu inatumia fursa hii kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa sera ya fedha na mchango wake katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha uchumi wa Taifa.

Aidha, wananchi wanaelimishwa kuhusu namna ya kuwekeza katika dhamana za serikali za muda mfupi na muda mrefu, ambazo ni miongoni mwa njia salama za kuwekeza mitaji.
BoT pia inatoa elimu kuhusu mifumo ya malipo ya taifa inayowezesha miamala kufanyika kwa haraka, ufanisi na usalama, sambamba na maelezo kuhusu namna taasisi hiyo inavyosimamia sekta ya fedha ili kuhakikisha taasisi za kifedha zinatoa huduma kwa mujibu wa sheria na kwa maslahi ya wananchi.

Wananchi wanaotembelea banda la Benki Kuu wanaelezwa pia kuhusu utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha, masuala ya ajira na utumishi ndani ya Benki Kuu, pamoja na fursa za masomo zinazotolewa na Chuo cha BoT kwa lengo la kukuza ujuzi katika nyanja za fedha na kibenki.
Aidha, elimu maalum inatolewa kuhusu alama za usalama katika noti halali za Tanzania na mbinu sahihi za kutunza noti na sarafu ili kudumisha ubora wake na kuzuia upotevu wa fedha taslimu.

Kupitia maonesho haya, Benki Kuu inaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kuelimisha umma, kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha zilizo salama, pamoja na kuchangia katika kujenga uchumi jumuishi na imara kwa maendeleo ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news