Rais Dkt.Mwinyi aishukuru China kwa ushirikiano katika Sekta ya Afya

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameshukuru Serikali ya China kwa ushirikiano mkubwa katika sekta mbalimbali, hususan Sekta ya Afya.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa shukrani hizo leo Agosti 25,2025 Ikulu, Zanzibar alipokutana na Timu ya 34 ya Madaktari Bingwa wa Kichina pamoja na Timu ya Wataalamu wa Kudhibiti na Kukinga Maradhi ya Kichocho waliomaliza muda wao wa kazi nchini.

Aidha, ameipongeza timu hiyo kwa kazi kubwa na ya mfano waliyoifanya katika kuwahudumia wananchi wa Unguja na Pemba, hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa kichocho.
Vile vile, Rais Dkt. Mwinyi amefarijika kwamba mbali na kutoa matibabu, madaktari hao pia waliwajengea uwezo watendaji wa sekta ya afya na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa.

Ameihakikishia Serikali ya China kuwa Zanzibar itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu baina ya pande hizo mbili, na imekuwa tayari kuikaribisha Timu ya 35 ya Madaktari Bingwa wa Kichina ambayo tayari imewasili nchini kuanza kutoa huduma.

Naye Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, amesema kuwepo kwa madaktari hao nchini ni uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na kumeokoa maisha ya wananchi wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mngereza Mzee Miraji, amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika kupunguza kiwango cha kichocho Unguja na Pemba, ambapo zaidi ya wagonjwa 40,000 wamehudumiwa, huku wagonjwa 13,000 wakilazwa na kufanyiwa upasuaji na madaktari hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news