ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejivunia kuwa mwenyeji mwenza wa Mkutano wa Dunia wa Miji na Maeneo Salama duniani.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Mohamed Mussa amesema, tukio hilo ni la kihistoria kwani linaashiria hatua madhubuti katika safari ya kuhakikisha usawa wa kijinsia na usalama wa wanawake na wasichana mijini.Meya alisisitiza kuimarisha ahadi kwa mustakabali Usio na Vurugu kwa Wanawake na Wasichana, akibainisha kuwa ni mwongozo wa utekelezaji kwa kila mji, kiongozi na raia. Aidha, aliishukuru UN Women, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, pamoja na wadau wa kimataifa kwa ushirikiano wao uliofanikisha mkutano huo.
Mkutano huo ulihitimishwa kwa mafanikio makubwa ambapo zaidi ya Mameya 50 kutoka miji mbalimbali duniani waliungana na Zanzibar katika kutia saini ahadi ya pamoja ya kuhakikisha miji salama na jumuishi. Meya alitangaza rasmi kuwa kuanzia Agosti 21, 2025, Jiji la Zanzibar limechaguliwa kuwa kitovu cha kuratibu mpango wa UN Women kwa nchi wanachama kupitia programu ya Miji salama.
Katika hotuba yake, alieleza dhamira ya Zanzibar kuendeleza upangaji wa miji unaozingatia usawa wa kijinsia, kuongeza usalama wa maeneo ya umma na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kupitia jukwaa la Miji salama.
Pia, alibainisha miradi inayotekelezwa kwa kushirikiana na vijana na wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa ufadhili wa Youth Climate Action Fund na Bloomberg Philanthropies.
Aidha, mameya kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Guinea, Niame, Colombia na Bolivia walishiriki kuwasilisha uzoefu na ubunifu wa nchi zao katika kupambana na ukatili wa kijinsia, kuimarisha miundombinu, na kukuza ushiriki wa wanawake kwenye upangaji miji. Vilevile, walijadili ushirikiano wa baadaye kati ya Zanzibar na nchi hizo katika nyanja za biashara, uchumi wa buluu, na mabadilishano ya mifumo ya kijamii.
Meya aliwataka washiriki waendelee kushirikiana kwa kueneza ujumbe wa mshikamano na matumaini, akibainisha kuwa urafiki uliotengenezwa Zanzibar uwe chachu ya miradi ya pamoja katika biashara, ujasiriamali, na ujenzi wa miji salama duniani kote.






