NA LWAGA MWAMBANDE
RAIS wa Sauti ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania (VOWET) na Mkurugenzi Mtendaji wa IBRA Construction Limited, Bi.Maida Waziri amewataka vijana kutambua kuwa, elimu haina maana kama haiwezi kutengeneza fursa,kipato au mabadiliko.
Bi.Waziri ameyabainisha hayo kupitia andiko alilochapisha katika ukurasa wake wa Instagram huku akisisitiza kuwa,kazi kubwa ni kugeuza elimu kuwa thamani katika maisha na jamii.Kwa msingi huo,mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,usia wa Bi.Maida Waziri kwa vijana umebeba ujumbe muhimu ikizingatiwa kuwa,elimu inakuwa na mashiko zaidi iwapo kila mmoja atatumia maarifa juu ya ujuzi alioupata ili kuwa na mbinu stahiki ya kuhamisha maarifa hayo katika utendaji na yakaleta matokeo chanya kwake na jamii. Endelea;
1:Dada Maida Waziri, vijana awausia,
Msikilize vizuri, na yake kuzingatia,
Wala msijefikiri, hapo mmemalizia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
2:Soma upate msonge, unaweza furahia,
Lakini vema jipange, hapo ni pa kuanzia,
Elimu yake ilenge, nafasi kukupatia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
3:Ukimaliza masomo, hili vema zingatia,
Siyo kufikia kimo, ukae kushangilia,
Jipatie hili somo, hapo ni pa kuanzia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
4:Elimu bure kabisa, isipokusaidia,
Wala kukupa hamasa, kipato kujipatia,
Unabakia garasa, huku unalialia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
5:Kama umeelimika, mabadiliko pitia,
Ulipo haujafika, ni ngazi pa kupandia,
Hiyo faida hakika, mema ukijipatia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
6:Geuza elimu yako, thamani kuipatia,
Ya kwamba maisha yako, ulipo sijebakia,
Kwa kuendelea kwako, pazuri umefikia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
7:Elimu futa ujinga, ufahamu waingia,
Kusaidia kupanga, mazuri kujifanyia,
Pazuri uweze tinga, chini ukiangalia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
8:Sema umeelimika, bure unajikalia,
Mimi ninachakarika, elimu naitumia,
Utabakia kuchoka, miaka ukijutia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
9:Wewe ni mwanasheria, shika kesi simamia,
Seremala angalia, samani twahitajia,
Utaalamu tumia, uweze kufaidia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
10:Elimu macho fungua, huku huko angalia,
Pagumu tapafungua, mema ukajipatia,
Huko hasa ni kukua, maisha kufurahia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
11:Huyu Maida Waziri, jina kubwa nakwambia,
Yeye afanya vizuri, elimu akitumia,
Hivyo sikiza vizuri, yake ya kushikilia,
Elimu faida yake, ni kutengeneza fursa.
12:Sema umeelimika, fursa ukijipatia,
Ila hujaelimika, ulipo ukitulia,
Umelalalala amka, uwezo wako tumia,
Elimu faida yake ni kutengeneza fursa.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
