DAR-Viongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wamefanya ziara ya ukaguzi katika miradi mikubwa ya ujenzi inayotekelezwa na shirika hilo ikiwemo wa Samia Housing II katika eneo la Kijichi, pamoja na mradi wa kisasa wa Boulevard uliopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, viongozi wamepata maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Mradi,Mhandisi John Edward, ambaye ameeleza hatua zilizofikiwa na kazi zinazoendelea.
Aidha, Afisa Mkuu wa Mauzo na Masoko, Bw. Daniel Kure ameeleza mipango ya mauzo na namna shirika linavyopanga kuyafikisha makazi hayo sokoni.
Vilevile, Msanifu Majengo, Bi. Julieth Prosper, amewasilisha mpango wa jumla wa ujenzi akibainisha kuwa awamu ya kwanza inahusisha majengo matano yenye jumla ya nyumba 100, huku awamu ya pili ikitarajiwa kuongeza majengo mengine saba na kufanya jumla ya nyumba kufikia 260.
Wakati wa ziara hiyo, viongozi wameshuhudia kazi mbalimbali za ujenzi zikiendelea kwa kasi na kwa viwango vya kitaalamu. Kazi hizo zimehusisha kumwaga blinding kwa Block E, maandalizi ya blinding level kwa Block D, marekebisho ya level ya Block C, na uchimbaji wa msingi wa Block A.
Pia maandalizi ya eneo la tenki la maji yameanza, hatua itakayohakikisha wakazi wa baadaye wanapata huduma ya maji ya uhakika.
Kwa upande wa Block B, timu ya wahandisi imekamilisha setting out za pad blinding na kuanza uchimbaji wa deeper pads. Shughuli za usafi wa jumla pia zilifanyika ili kulinda usalama na mwonekano wa mradi.
Mbali na Samia Housing II-Kijichi, viongozi hao wametembelea pia mradi wa Boulevard Residences, uliopo katika kiwanja namba 105, ambapo walielezwa kuwa jengo hilo litakapokamilika litakuwa na jumla ya nyumba 70 zikiwemo nyumba 35 za kupangisha na nyumba 35 za kuuzwa,zote zikiwa za hadhi ya juu.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Meneja Mauzo na Masoko wa NHC, Bw. Deogratius Batakanwa amesema kuwa, lengo la kuandaa ziara hiyo ni kuwajengea viongozi uelewa wa moja kwa moja ili wawe mabalozi wa shirika kwa wananchi katika kuuza nyumba hizo."Lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, salama na yenye huduma muhimu. Ndiyo maana tunasimamia kila hatua ya mradi kwa umakini mkubwa ili ukamilike kwa viwango vya juu na ndani ya muda uliopangwa,"amesema Bw. Batakanwa.
Kwa upande wake, Meneja Ukusanyaji Madeni wa NHC, Bw. Leviniko Mbilinyi amepongeza maandalizi ya ziara hiyo na kusisitiza kuwa mikutano ya aina hiyo ina maana kubwa, kwani inawawezesha wafanyakazi na viongozi kushuhudia changamoto zilizopo na kutoa maoni ya maboresho, hali inayosaidia Shirika kukamilisha miradi yenye ubora wa hali ya juu.
Mradi wa Samia Housing II-Kijichi ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kupitia NHC wa kuongeza upatikanaji wa makazi bora, ya kisasa na yenye huduma zote muhimu jijini Dar es Salaam.
Ukikamilika, mradi huu unatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa wananchi wanaotafuta nyumba zenye miundombinu rafiki na viwango vya kisasa vinavyokidhi mahitaji ya maisha ya leo.
Kwa hatua hii, NHC inaendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, ya uhakika na yenye hadhi.


