DAR-Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dkt. Germana Leyna ametoa wito kwa wadu wa masuala ya lishe nchini kuendelea kuunga mkono jitihada za kupambana na changamoto zinazokabili masuala ya Lishe huku akisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabili changamoto hizo kwa kuwa na mikakati madhubuti.
Wito huo umetolewa leo Septemba 29, 2025 kwenye mahojiano maalumu katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) jijini Dar es Salaam katika kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa 11 wa Wadau wa Masuala ya Lishe.
"Serikali imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa wa masuala ya lishe ili kuendelea kuwa na Taifa lenye watu wenye lishe bora na niseme hapa kuwa wadau waje tuunganishe nguvu katika kupambana na changamoto za masuala ya lishe," amesema Dkt.Germana Leyna.
Pia, ameongoza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inawafikia wazalishaji hasa wakulima wawapo katika shughuli zao za kilimo na kuhakikisha wanapata elimu ya lishe bora na umuhimu wa kutunza chakula cha matumizi ya nyumbani badala ya kuuza chote.
Ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wadau kuendelea kujitokeza na kuendelea kuweka chachu katika masuala ya lishe nchini.



