Wakaguzi wa Ndani wavutiwa na huduma za NHC

ARUSHA-Banda la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kando ya Mkutano wa 18 wa wakaguzi wa ndani wa Serikali na taasisi binafsi limeendelea kuwa kivutio kwa wadau mbalimbali wanaoshiriki mkutano huo.Mkutano huo ambao unahudhuriwa na watu zaidi ya 3,000 kutoka ndani na nje ya nchi unaendelea katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.

Kupitia banda maalum la maonesho, NHC inawapatia washiriki wa mkutano huo ambao wengi wao ni wataalamu wa ukaguzi na usimamizi wa fedha fursa ya kuelewa kwa kina dhamira, mikakati na utekelezaji wa miradi ya shirika nchini.

Miongoni mwa miradi hiyo ni iliyopo na inayoendelea ikiwemo 711 (Dar), Medeli III, Uluguru Plaza, Kijichi Residence (Samia Housing Scheme phase II) jijini Dar es Salaam, Sokoine Square (Arusha) na viwanja vya Safari City jijini Arusha.
Aidha, kwa kufanya hivyo, NHC ambao wamedhamini mkutano huo, inajenga uelewa mpana wa jamii ya kitaaluma kuhusu mchango wake katika uboreshaji wa maisha ya wananchi kupitia ujenzi wa nyumba bora, za kisasa na zenye kuendana na mahitaji ya wakati huu.

Vilevile, shirika linaweka wazi jinsi linavyotekeleza miradi kwa kuzingatia misingi ya uwazi, ufanisi na uadilifu ambayo pia inahimizwa na taaluma ya ukaguzi wa ndani.

Kwa NHC, mkutano huu si jukwaa la kawaida, bali ni fursa ya kuwasiliana moja kwa moja na wataalamu wa ukaguzi, kupata mrejesho, kujenga uaminifu na kuendeleza ushirikiano kati ya taasisi za umma katika kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa tija na manufaa ya Watanzania wote.
Kwa kutambua nafasi ya ukaguzi wa ndani kama nguzo muhimu katika kusimamia rasilimali, kuboresha mifumo ya udhibiti wa ndani, na kuhakikisha uwazi katika uendeshaji wa taasisi, NHC limeona ni wajibu wake kuunga mkono jukwaa hili muhimu la kitaaluma.

Aidha,kupitia udhamini huu, NHC haijajitokeza tu kama mshiriki wa maendeleo ya kitaifa, bali pia kama mdau wa kweli katika kuimarisha utendaji wa taasisi kwa kuzingatia kanuni bora za usimamizi wa fedha, miradi na mali za umma.

Ukaguzi wa ndani ulio bora unahusiana moja kwa moja na uendelevu wa taasisi, jambo ambalo linagusa pia msingi wa kazi wa NHC kama taasisi inayojikita katika utoaji wa huduma za makazi bora na endelevu kwa Watanzania.
Udhamini huu unaakisi maono ya NHC ya kuona taasisi za umma na binafsi zikiwa thabiti, zenye kuwajibika na zenye kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa manufaa ya taifa zima.

NHC lina jukumu la kujenga nyumba za makazi na majengo mengine kwa ajili ya kuuza na kupangisha nchini.
Vilevile,shirika linajenga majengo kulingana na mipango iliyoidhinishwa na Serikali na juzalisha na kuwezesha uzalishaji wa vifaa vya ujenzi.

Jambo lingine ni kusimamia miliki za majengo yake na ya wamiliki wengine ikiwa ni pamoja na kuyafanyia matengenezo na kukusanya kodi za pango.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here