WASHINGTON-Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, aliongoza Ujumbe wa Tanzania katika kikao na IFC - International Finance Corporation kilichokuwa chini ya Mkurugenzi wa Taasisi hiyo anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Mary Peschka ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili kuhusu ushirikiano uliopo kati ya taasisi hiyo iliyo chini ya Benki ya Dunia na Tanzania.
Miongoni mwa masuala muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na taasisi hiyo kushirikiana na Tanzania kutekeleza programu mpya ya kuendeleza kilimo biashara (AgroConnect), kuendeleza nishati safi, na ya gharama nafuu kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendelo 2050, kuendeleza sekta binafsi na masuala ya fedha kwa ujumla.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Kanza, Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, Kamishna Msaidizi kutoka Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bw. Nathan Belete na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Benki ya Dunia.







