Dkt.Mwinyi aahidi Tume Maalum ya kuhakiki fidia kwa wananchi waliolipwa kupisha miradi ya maendeleo

ZANZIBAR-Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kuunda Tume Maalum itakayofanya tathmini ya kina kuhusu fidia walizolipwa wananchi waliopisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo ya Fumba, Nyamanzi, Dimani na Bweleo ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake stahiki.
Dkt.Mwinyi amesema,tume hiyo itapitia na kuhakiki fidia zote zilizolipwa kwa wananchi kwa lengo la kujiridhisha kuwa kila anayestahiki amelipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Ametoa ahadi hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Michezo wa Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi leo Oktoba 14, 2025 ambapo wananchi wengi walieleza kutoridhika na fidia walizopokea baada ya kupisha miradi ya uwekezaji na maendeleo katika maeneo yao.
Rais Dkt. Mwinyi amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kudhibiti udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watu wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo kujenga haraka au kuotesha miti kwa lengo la kudai fidia, jambo ambalo halikubaliki kisheria.

Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali na yeye binafsi hawataridhia mtu yeyote kudhulumiwa, na kila anayestahiki atalipwa fidia yake kwa mujibu wa eneo analomiliki. Amesema lengo la Serikali ni kuwaondoa wananchi katika umasikini, si kuwatia umasikini.

Pia,Dkt.Mwinyi ameagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu kabla ya kutekelezwa kwa miradi yoyote ya maendeleo, sambamba na kupiga picha za maeneo husika ili kuweka kumbukumbu sahihi zitakazosaidia kuepusha migogoro ya ardhi.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa kipindi kingine tena, ili aweze kukamilisha utekelezaji wa ahadi zake na kuleta maendeleo makubwa zaidi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Muhammed Said Dimwa, amesema Chama hakikukosea kumteua Dkt. Mwinyi kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar, akieleza kuwa ni kiongozi mzalendo, mtekelezaji wa ahadi na mwenye dira ya maendeleo ya kweli kwa Taifa.

Wananchi waliopata nafasi ya kutoa hoja zao katika mkutano huo wamemshukuru Dkt. Mwinyi kwa kutekeleza kwa kiwango kikubwa ahadi zake zilizosaidia kupunguza changamoto nyingi za kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news