Zambia kuuza nyama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,kuvuna dola bilioni 1

LUSAKA-Wafugaji katika Wilaya ya Namwala iliyopo Mkoa wa Kusini mwa Zambia wameanza kusafirisha ng’ombe kwa ajili ya kuchinjwa ili nyama ikauzwe Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hatua ambayo ni muhimu katika jitihada za Zambia za kukuza mauzo ya bidhaa zisizo za kawaida katika masoko ya Kimataifa.
Wiki hii, tani 40 za nyama ya ng’ombe zinapelekwa nchini DRC kama sehemu ya kundi la awali la usafirishaji.

Kelvin Puuka kutoka Dodo Beef Compartment ametoa ng’ombe 25 kwa ajili ya kuandaliwa nyama ambayo itasafirishwa kwenda kuuzwa DRC.

Bw.Puuka ambaye alikuwepo wakati wa kupakia ng’ombe wake, ameishukuru Serikali kwa kufungua masoko ya kimataifa kwa wazalishaji wa nyama ya ng’ombe wa Zambia, akiongeza kuwa, hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa wafugaji wa maeneo ya vijijini.

Naye Dkt.Harrison Chiwawa ambaye ni Mratibu wa Samaki na Mifugo Wilaya ya Namwala, amethibitisha kuwa ng’ombe hao watapelekwa Kalomo kwa ajili ya kuchinjwa kabla ya kusafirishwa.

Amesisitiza kuwa, mifugo hiyo inakidhi viwango vya kimataifa vya usafirishaji na ni yenye ubora wa hali ya juu.

Idara ya Mifugo nchini Zambia imefanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magonjwa na kuthibitisha kuwa, mifugo na vituo vya kuchinjia ni salama na haina magonjwa.

Rais Hakainde Hichilema wa Zambia ameweka lengo la kujenga sekta ya mauzo ya nyama ya ng’ombe yenye thamani ya dola bilioni 1, kama sehemu ya mkakati mpana wa kuongeza utofauti wa uchumi wa Zambia na kuimarisha ushawishi wa nchi katika biashara ya kimataifa.

Aidha,hatua hii ni ishara ya kuongezeka kwa imani ya wawekezaji na masoko katika sekta ya mifugo ya Zambia, na pia ni fursa kubwa ya kuongeza mapato, kuunda ajira na kuendeleza maendeleo ya maeneo ya vijijini. (znbc)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news