NA DIRAMAKINI
KLABU ya Young Africans Sports Club (Yanga SC) imemteua Filipe Duarte da Silva Pedro raia wa Ureno kuwa Kocha Msaidizi ambaye atasaidiana na Kocha Mkuu wa klabu hiyo,Pedro Goncalves.
Ujio wa kocha huyo unalenga kuimarisha mbinu za mafunzo, maendeleo ya wachezaji, na mikakati ya kiufundi ya timu katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.
Filipe Pedro mwenye umri wa miaka 38 ana leseni ya UEFA Daraja la A na ana uzoefu mkubwa katika klabu za vijana na timu za wakubwa.
Kabla ya kujiunga na Yanga SC, aliwahi kuwa kocha wa timu ya vijana ya Sporting Clube de Portugal (U19), moja ya akademi bora zaidi barani Ulaya inayojulikana kwa kukuza wachezaji nyota duniani.
Kwenye majukumu yake mapya, Pedro atafanya kazi kwa karibu na kocha mkuu wa Yanga SC, akijikita katika kuimarisha uchambuzi wa mchezo na wapinzani,kuandaa programu za mafunzo ya wachezaji kulingana na viwango vya kimataifa.
Pia,kutumia teknolojia ya kisasa ya michezo katika upangaji na tathmini ya mazoezi, kocha huyo anatajwa kuwa mwalimu mwenye ujuzi na nidhamu ya hali ya juu.
Tags
Filipe Pedro
Habari
Kocha Msaidizi Yanga SC
Michezo
Young Africans SC
Young Africans Sports Club
