KILIMANJARO-Mahakama ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro chini ya Hakimu Mkuu Mwandamizi, Mheshimiwa Innocent Nyella imemkuta na hatia fundi bomba wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Rombo (ROMBOWSSA), Bw. Hemrod Elias Ngunga kwa kosa la kushawishi,kuomba na kupokea hongo.
Picha na mtandao.
Katika kesi ya jinai namba 9081/2025, Bw. Ngunga alishtakiwa na Jamhuri kwa makosa yanayokiuka vifungu vya 15(1)(a)(b) na (2) vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya Mwaka 2022.
Kwa mujibu wa mawakili wa serikali,Bi. Furahini Kibanga na Bw.Anold Mafwele, mshtakiwa akiwa mtumishi wa ROMBOWSSA alitenda kosa hilo kwa kuomba na kupokea hongo ya shilingi 20,000 kutoka kwa mteja ili kumsaidia kurejeshewa mita zake za maji zilizokuwa zimeibiwa katika eneo la Holili.
Aidha,baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za pande zote, Mahakama ilimkuta Bw.Ngunga na hatia na kumhukumu kulipa faini ya shilingi 300,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kulipa faini hiyo na hivyo amepelekwa rumande kuanza kutumikia kifungo chake.
.jpeg)