NA DIRAMAKINI
KATIKA hatua inayodhihirisha mafanikio ya juhudi za kiuchumi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeipongeza nchi kwa matumizi bora na usimamizi wa fedha unaoleta matokeo chanya.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni jijini Washington D.C nchini Marekani na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa IMF, Bw.Adran Ubisse wakati wa mazungumzo rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba.
Katika mkutano huo, Dkt. Mwamba alielezea jinsi Tanzania inavyoendelea kuimarika kiuchumi, ambapo ukuaji wa pato la taifa umefikia asilimia 5.8 katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 ukilinganishwa na asilimia 5.2 mwaka uliotangulia.
Alisisitiza kuwa, mafanikio hayo yanatokana na usimamizi thabiti wa sera za uchumi na fedha, pamoja na kuimarika kwa sekta kama vile madini, nishati na huduma za kifedha.
Aidha, mfumuko wa bei umeendelea kubaki kwenye tarakimu moja, hali inayoonyesha uthabiti wa uchumi wa ndani.
IMF imeitaja Tanzania kuwa mfano wa kuigwa kwa matumizi sahihi ya fedha za mikopo na utekelezaji madhubuti wa miradi ya maendeleo.
Pongezi hizi kutoka IMF si tu heshima kwa Tanzania, bali pia zinafungua milango ya fursa mpya za kifedha na kiuwekezaji.
Vilevile,zinathibitisha kuwa, sera bora, uwazi na uwajibikaji vinaweza kuleta maendeleo ya kweli.
Hii ni hatua muhimu kwa nchi, kwani inajenga imani ya kimataifa na kuvutia wadau zaidi kuwekeza na kushirikiana na Tanzania katika safari yake ya kuleta ustawi bora kwa wananchi wote.
Bila shaka, huu ni ushindi wa kiuchumi unaopaswa kuenziwa na kuendelezwa chini ya uongozi thabiti wa Rais Dkt.Samia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) anayesimamia Idara ya Afrika,Bw.Abebe Selassie amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vema sera za uchumi na fedha za nchi yake.
Vilevile kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na namna anavyosimamia fedha za miradi zinazotolewa na taasisi hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika.
Bw.Abebe amesema kuwa,Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha ambapo licha ya changamoto za UVIKO-19 na mizozo ya kisiasa inayoendelea sehemu mbalimbali duniani, tathimini ya shirika hilo inaonesha kuwa,uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha,Dkt.Mwamba aliishukuru IMF kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi kupitia misaada, mikopo nafuu na misaada ya kiufundi pamoja na miongozo mbalimbali inayoipatia nchi hatua iliyosaidia kuimarisha uchumi wa nchi.
Awali,timu ya wataalamu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ikiongozwa na Bw. Nicolas Blancher ilikuwa na ziara yake nchini Tanzania.
Ziara hiyo ilifanyika kuanzia Septemba 17 hadi 24, 2025, ambapo ilifanya tathmini ya mwenendo wa hali ya uchumi, matarajio ya kiuchumi na utekelezaji wa programu za mageuzi.
Bw.Blancher katika taarifa iliyochapishwa katika tovuti rasmi ya shirika hilo alisema kuwa, baada ya ziara yao, wameona uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa thabiti zaidi.
Pia,amesema umekua kwa asilimia zaidi ya 5 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kuanzia Julai hadi Septemba,huku mfumuko wa bei ukibaki katika kiwango cha chini cha asilimia 3.4 mwezi Agosti.
Mtaalamu huyo kutoka IMF amebainisha kuwa, sekta za madini, kilimo, viwanda na ujenzi ndizo zimekuwa nguzo kuu za ukuaji huo.
IMF ilibainisha kuwa, kuna matarajio chanya ikiwemo mageuzi ya mapato kupitia Mkakati wa Muda wa Kati wa Mapato (Medium-Term Revenue Strategy) ambapo yanatarajiwa kuongeza kupitia ukusanyaji wa mapato na kuwezesha uwekezaji zaidi katika sekta za kijamii.
“Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ndani ya kiwango cha lengo la asilimia 3 hadi 5, na hatua ya kupunguza riba ya Benki Kuu hadi asilimia 5.75 imesaidia kuchochea shughuli za kiuchumi."
Bw.Blancher aliongeza kuwa, uboreshaji wa soko la fedha za kigeni umeongeza ukwasi na kupunguza tofauti kati ya soko rasmi na lisilo rasmi.
Pia,nakisi ya akaunti ya sasa imeshuka hadi asilimia 2.5 ya Pato la Taifa katika mwaka wa fedha 2024/25, ikichangiwa na mauzo ya madini, bidhaa za kilimo na utalii.
Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 6.2 kufikia Julai 2025, sawa na zaidi ya miezi minne ya uagizaji bidhaa.
IMF imesisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa mageuzi ili kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, ikiwa ni pamoja na kuwekeza kwenye elimu, afya, ajira kwa vijana na mageuzi ya tabianchi kupitia msaada wa washirika wa maendeleo.
IMF pia imetoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia kwa ukarimu na majadiliano yenye mafanikio wakati wa ziara hiyo.
Pongezi za IMF kwa Tanzania juu ya matumizi na usimamizi bora wa fedha zina manufaa muhimu, kiuchumi na kidiplomasia.
Mosi, IMF inapotoa pongezi, inaleta ujumbe mzuri kwa taasisi nyingine za kifedha na nchi wahisani kuwa Tanzania ni nchi inayoaminika kutumia fedha kwa ufanisi.
Hatua hii inaweza kuvutia misaada zaidi ya kifedha, kiufundi na kuongeza uwezekano wa kupunguziwa masharti ya mikopo au kupata mikopo yenye masharti nafuu zaidi.
Pili,pongezi kutoka IMF ni ishara ya uthabiti wa sera za uchumi. Hii inaweza kuwahamasisha wawekezaji wa kimataifa kuwekeza nchini,kwani mazingira ya kifedha ni salama.
Aidha,inasaidia wawekezaji wa ndani kuwa na imani ya kuendeleza biashara bila hofu ya misukosuko ya kiuchumi.
Tatu,pongezi hizo zinaweza kuwa motisha kwa serikali kuendelea na usimamizi mzuri wa fedha za umma na kuepuka ubadhirifu au matumizi yasiyo na tija.
Pia zinasaidia kuimarisha uwajibikaji na uwazi kwa umma na zinaboresha nafasi ya Tanzania katika viwango vya kimataifa vya tathmini ya uchumi na utawala wa kifedha.
Kwa ujumla, pongezi hizi ni ishara ya uaminifu wa kimataifa na zinaweza kuimarisha zaidi maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Aidha, hatua hii inaonesha kuwa mwelekeo wa Serikali ya Tanzania katika kujenga uchumi wa kisasa na shindani ni sahihi.
Ni ushahidi kuwa usimamizi mzuri wa fedha si tu suala la nadharia, bali ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kweli.
Hii ni nafasi ya kuendeleza mafanikio haya kwa kuhakikisha kuwa nidhamu ya matumizi ya fedha inaimarishwa zaidi, miradi inaleta tija kwa wananchi, na kila fedha inayotumika inaleta matokeo chanya.
Kwa muktadha huo,Tanzania sasa ipo katika nafasi nzuri ya kuandika sura mpya ya mafanikio ya kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Tanzania ni mwana hisa wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia na ushiriki wake katika Mikutano hiyo unalenga kulinda na kutetea maslahi ya nchi katika mashirika hayo makubwa ya fedha duniani kwa kushiriki mikutano ya kiutawala na kiuendeshaji.
