DAR-Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetoa taarifa rasmi kuhusu ajali iliyohusisha treni ya kisasa ya EMU iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma, majira ya saa 2:00 asubuhi ya leo Oktoba 23, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ajali hiyo imetokea katika kituo cha Ruvu na imetokana na hitilafu za kiuendeshaji. Hata hivyo, taarifa za awali zinaeleza kuwa hakuna tukio la kifo lililoripotiwa kufuatia ajali hiyo.
TRC imeeleza kuwa tayari timu ya wataalamu imeanza uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo. Timu hiyo inaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama na menejimenti ya TRC.
Aidha,shirika limewahakikishia wananchi kuwa juhudi zinaendelea kufanyika ili kurejesha huduma kwa haraka na kuhakikisha usalama wa abiria unaendelea kupewa kipaumbele.

