Zanzibar yaweka rekodi chanya ya ukuaji kiuchumi

NA GODFREY NNKO

UCHUMI wa Zanzibar umeonesha dalili thabiti za ustawi, baada ya kukua kwa asilimia 6.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ukuaji ambao ni sawa na ule ulioshuhudiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba ambaye pia ni Gavana wa BoT ameyasema hayo leo Oktoba 02,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika mkutano na viongozi wa benki, taasisi za fedha na waandishi wa habari.

Gavana Tutuba alikuwa akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ilikutana Oktoba 1,2025 na kuamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 5.75 kwa robo ya nne ya mwaka 2025 kama ilivyokuwa kwa robo ya tatu iliyoishia mwezi Septemba,2025.

Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) ni kiwango kinachowekwa na BoT kama rejea katika utekelezaji wa shughuli zake mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukopesha benki za biashara.

Aidha,kiwango hiki huathiri riba za mikopo baina ya benki za biashara, ambazo zinapaswa kuwa ndani ya wigo wa asilimia ±2.0 ya CBR iliyowekwa.
Gavana Tutuba amesema, ukuaji wa uchumi wa Zanzibar umetokana na ongezeko la shughuli za utalii, sekta ya ujenzi, pamoja na maendeleo katika kilimo.

Katika mtazamo mpana wa mwaka mzima, uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.3 ifikapo mwisho wa 2025 ikiwa ni ishara chanya ya kuimarika kwa mazingira ya biashara, uwekezaji na sera madhubuti za kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi.

Vilevile,katika upande wa ustawi wa kijamii, mfumuko wa bei umepungua kutoka asilimia 4.2 hadi asilimia 4.0, na kubaki ndani ya lengo la sera ya fedha, kutokana na kupungua kwa bei za vyakula, jambo linalotoa unafuu mkubwa kwa wananchi wa kipato cha chini na la kati.

Gavana Tutuba amebainisha kuwa,matarajio ya mfumuko wa bei ni kuendelea kubaki chini ya lengo la asilimia 5 katika kipindi kijacho, hali inayotoa mazingira bora kwa maisha ya wananchi na shughuli za kiuchumi.

Aidha,kwa upande wa mizania ya malipo, Gavana Tutuba amesema, Zanzibar imepiga hatua kubwa.

Pia, Gavana Tutuba amesema, ziada ya urari wa malipo ya kawaida Zanzibar imeongezeka hadi Dola za Marekani milioni 685.6 kwa mwaka ulioishia Septemba 2025, kutoka Dola milioni 499.0 mwaka uliopita.

Amesema,ongezeko hilo limetokana na mapato ya huduma, hususan kutoka sekta ya utalii, ambayo inaendelea kuwa nguzo muhimu ya mapato ya kigeni na ajira.
Hata hivyo, takwimu hizi zinadhihirisha mwelekeo chanya wa uchumi wa Zanzibar na mafanikio ya sera za serikali katika kukuza uchumi jumuishi unaowanufaisha wananchi wote.

Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, utekelezaji wa bajeti za Serikali katika robo ya kwanza ya mwaka 2025/26 ulikuwa wa kuridhisha kwa Tanzania Bara na Zanzibar. 

Mapato ya ndani yalivuka lengo kutokana na mwenendo mzuri wa makusanyo ya kodi kufuatia kuongezeka kwa utayari katika ulipaji wa kodi kwa hiyari, sambamba na usimamizi thabiti. 

Matumizi ya Serikali yaliendelea kuoanishwa na rasilimali zilizopo, hali inayoakisi usimamizi madhubuti wa fedha za umma. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news