Rais Dkt.Mwinyi akagua maendeleo ya ujenzi wa Zanzibar Sports City kuelekea AFCON 2027

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Zanzibar Sports City unaotekelezwa katika eneo la Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Michezo ya AFCON 2027.
Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi aliihakikishia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo pamoja na Kampuni ya ORKUN GROUP kuwa Serikali imefungua milango kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kwa kasi, ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Aidha, aliitaka Wizara na mkandarasi kutowasilisha changamoto kwa kuchelewa, ili Serikali iweze kutoa ufumbuzi wa haraka pale unapohitajika.
Rais Dkt. Mwinyi aliambatana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Riziki Pemba Juma, pamoja na Naibu Waziri, Mhe. Ali Abdulgullam Hussein, katika ziara iliyofanyika leo tarehe 18 Novemba 2025.

Mradi wa Zanzibar Sports City ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya michezo na kukuza maendeleo ya sekta hiyo nchini.
Awamu ya kwanza ya mradi huo inajumuisha ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Mpira wa Miguu wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 36,500, pamoja na viwanja viwili vya mazoezi vyenye uwezo wa kuchukua mashabiki 15,000 kila kimoja. Moja ya viwanja hivyo pia kitatumika kwa ajili ya sherehe za Kitaifa.

Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba 2026.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news