NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Tanzania imekemea vikali kitendo kinachodaiwa kufanywa na Shirika la Habari la Kimataifa la CNN, ikikitaja kuwa ni ukiukaji mkubwa na wa makusudi wa misingi ya uandishi wa habari.


Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Bw. Gerson Msigwa ameyasema hayo leo Novemba 23,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Msigwa amesema, hatua za CNN, ambazo amedai zimetofautiana na misingi ya kitaaluma na maadili ya habari, pia zilifanywa na vyombo vingine vya kimataifa vikiwamo BBC, Al-Jazeera na Deutsche Welle.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa, mwenendo huo hauakisi viwango vinavyotakiwa katika utoaji wa taarifa sahihi na zenye uwajibikaji.
“Misingi na maadili ya uandishi wa habari ndiyo nguzo ya kufanya kazi kwa uwazi, usahihi na uwajibikaji. Kitendo hiki ni ukiukwaji mkubwa na wa makusudi,”amesema Msigwa huku akisisitiza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuzingatia taratibu za kitaaluma ili kulinda hadhi na uaminifu wa taaluma hiyo.
Ameongeza kuwa, Serikali haitachoka kukumbusha na kusisitiza umuhimu wa vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kufuata kanuni zinazoongoza uandishi wa habari, kwa kuwa taarifa zenye upotoshaji au zisizofuata maadili zina madhara makubwa kwa jamii.
TAARIFA YA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI LEO NOVEMBA 23,2025 JIJINI DAR ES SALAAM
Malengo ya mkutano
Ndugu Waandishi wa Habari tumekutana hapa leo kwa ajili ya jambo moja ambalo nimeona nimezungumze nanyi ili kueleza baadhi ya mambo yaliyojitokeza kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani ya tarehe 29 Octoba, 2025 na siku chache zilizofuata.
Nyote mtakumbuka kuwa tarehe 29 Oktoba, 2025 ilikuwa siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na Watanzania walijitokeza katika siku hii ili kutumia haki yao ya Kikatiba ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.
Naomba kuchukua nafasi hii kuwapongeza Watanzania wote kwa kutumia haki hii ipasavyo na hatimaye wamempata Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wabunge na Madiwani ambao wataongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
Halikadhalika nawapongeza kwa kujitokeza kwa wingi ambapo safari hii maandalizi mazuri yaliyofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania (INEC) na kwa kuwezeshwa fedha za uchaguzi na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.
Tumeona Watanzania wamejitokeza kwa wingi katika kupiga kura kuliko wakati mwingine wowote na waliweza kupiga kura na kumaliza kwa haraka kwa sababu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili jipanga vizuri iliandaa vituo vingi vya kupigia kura na zoezi lilikwenda kwa haraka.
Ndugu zangu Waandishi wa Habari.
Siku ya uchaguzi yaani tarehe 29 Oktoba, 2025 na siku chache zilizofuata kulijitokeza vitendo vya uvunifu wa amani ulioambatana na vurugu zilizokuwa zikifanywa na baadhi ya watu na ambazo zililazimu vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kukabiliana na vitendo hivyo.
Kufuatia vurugu hizo tumepata madhara yakiwemo vifo vya raia na askari, uharibifu mkubwa wa miundombinu ya umma na mali za watu binafsi, kuharibu biashara za watu na wizi.
Naomba kurudia kauli aliyoitoa Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutoa pole nyingi kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao na sote tuwaombee Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi, Amina.
Kadhalika naomba kuchukua nafasi hii kuwapa pole wote waliopata madhara mbalimbali yaliyotokana na vitendo vya vurugu zile ikiwemo kuumia, kupoteza mali zao na biashara zao, kupoteza ajira na madhara mangine ambayo siwezi kuyataja yote.
Mwenyezi Mungu ayaponye maumivu yenu na inshaalah awarejeshe tena mkiwa imara.
Tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya kuapishwa ameunda Tume Huru ya Uchunguzi wa matukio yaliyotokea siku ya uchaguzi na siku zilizofuata.

Tume hii inaongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mstaafu, Mheshimiwa Mohammed Chande Othman na itafanya kazi kwa miezi mitatu.
Ndugu zangu Waandishi wa Habari,
Tunapoendelea kusubiri Tume hii ifanye kazi yake na kuikamilisha, kumejitokeza wimbo kubwa la vyombo vya habari vya nje ya nchi kuchapisha na kutangaza taarifa ambazo ni za upande mmoja na wakati mwingine kufanya uposhaji wa taarifa hizo wenye mlengo wa kuchochea chuki kwa Watanzania dhidi ya Serikali, kugombanisha Watanzania wenyewe kwa wenyewe kutokana na tofauti za kisiasa, kidini na kikanda.
Naomba kurudia, Serikali ama viongozi wa Serikali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inasikitishwa na imeumizwa sana na matukio yale na madhara yake. Madhara haya yametugusa sote ama moja kwa moja ama kwa namna nyingine.
Kuendelea kuyashabikia matukio yale au kuchochea kwa kutangaza na kuchapisha maudhui yenye kuzua taharuki, kupotosha ama kutia hasira watu kwa namna ambavyo vyombo vya habari vya nje ya nchi, ama wanaharakati ama watu wenye maslahi ya kisiasa wanafanya hakuna manufaa kwa Taifa letu zaidi ya kuongeza maumivu katika vidonda vya watu.
Kutokana na hayo, kwa niaba ya Serikali naomba kueleza yafuatayo
Natoa wito kwa vyombo vya habari vya nje kuzingatia maadili na misingi ya uandishi wa habari kwa kuacha kuchapisha habari za upande mmoja zenye nia ovu kwa Watanzania na nchi yetu ya Tanzania.
Serikali ipo tayari wakati wote kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi pale watakapotaka taarifa.
Naomba kusisitiza sio haki na sio sawa kwa chombo cha habari kuchapisha taarifa za upande mmoja na kisha kutoa sababu kuwa maafisa wa Serikali walitafutwa hawakupatikana kama ambavyo chombo cha habari cha CNN kimechapisha taarifa zake zilizojaa tuhuma dhidi ya Serikali ya Tanzania pasipo kutoa nafasi ya Serikali kujibu.
Kitendo kichofanywa na CNN pia kimefanywa na vyombo vya habari vingine vya Kimataifa vikiwemo BBC, Aljazeerana DW.
Nasisitiza hii sio sawa, sio haki na katika misingi na maadili ya Uandishi wa Habari huu ni ukiukwaji mkubwa na wa makusudi.
Kwa kuwa Rais ameunda Tume Huru ya Uchunguzi, ni muhimu vyombo vya habari vikajiepusha kuingilia uchunguzi unaoendelea na kama kuna chombo cha habari kina taarifa za uchunguzi kiwasilishe kwa Tume ili taarifa hizo zizingatiwe katika ripoti pale kamati itakapokamilisha kazi yake.
Kwa Waandishi wa Habari wa Tanzania na Wahariri wenzangu wa Tanzania, naomba kuwapongeza kwa kufanya kazi zenu kwa weledi, umakini na kutanguliza maslahi ya Taifa.
Najua kuna magenge ya watu ambao wanashabikia nchi isambaratike yanawashambulia sana kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya nje ya nchi, nataka kuwatia moyo na kuwahakikishia mpo sahihi sana na mmeonyesha umuhimu wa Tanzania kwanza na upekee wa nchi yetu.
Leo mtabezwa lakini historia itaandika kuwa nchi iliwahi kupita kwenye mtikisiko na Waandishi wa Habari walisimamia maslahi ya Taifa na nchi ikabaki salama.
Endeleeni na msimamo huo. Kama nilivyosema nchi imepita katika changamoto ambazo sio nzuri kwa maslahi mapana ya Taifa.
Mnachokifanya ni “Uandishi wa Habari wa Uwajibikaji” yaani Responsible Journalism – Which embarks in reporting news accurately, fair and accountable.
That is verifying facts, avoiding bias and conflict of interest and being transparent about sources and mistakes.
Kwa Watanzania wote, naomba kuchukua nafasi hii kuwasihi kujiepusha kushabikia na kusambaza taarifa ama habari zinazochochea uhasama, hasira na kuvunja umoja wetu wa Kitaifa.
Naomba Watanzania, tung’amue mtego wa kuliangamiza Taifa letu. Tunapita kwenye kipindi ambacho tukiendekeza uchochezi unaofanywa na watu ambao wapo nje ya nchi na hawaguswi na chochote juu ya maisha yetu, wanaowashawishi vijana wetu kufanya vitendo vya kuumiza nchi yetu tutakaoumia ni sisi na tutaumia kweli tukifanya masihara.
Ni vizuri mjue kuwa tupo kwenye kipindi ambacho kwa kiingereza kinaitwa Information Warfare (yaani Vita vya taarifa).
Wasiotutakia kheri wanatumia mwanya wa upashanaji taarifa kutugombanisha, kutuchonganisha na kutufitinisha ili tukiharibikiwa waweze kupata maslahi yao, na kwa sehemu kubwa ni maslahi ya kisiasa na kiuchumi.
Wanatumia mkakati unaitwa “The weaponization of narrative” yaani wanatumia silaha ya kutengeneza simulizi ya Tanzania inayoonesha Tanzania ni nchi mbaya, nchi ya hatari, nchi isiyokuwa salama na nchi isiyofaa. Wanataka wageni wakiwemo wawekezaji, wafanyabiashara na watalii waogope kuja Tanzania.
Na naposema haya situngi maneno. Wote mtakuwa mmeona, kampeni za mtandaoni zilizoanzishwa kwa lengo kuathiri uchumi wetu, kuwatishia Watalii wasije Tanzania, Wanawatisha wawekezaji waogope kuwekeza Tanzania, Wanawatisha wafanyabiashara waogope kupitisha mizigo yao Tanzania na mengine mengi ambayo lengo lao ni kuangusha uchumi ili nchi iingie katika matatizo yatakayowaumiza Watanzania na kuwapa faida washindani wetu wa kiuchumi.
Baadhi ya mbinu hasi wanazotumia ni kutengeneza maudhui ya uongo na kusambaza mtandaoni, mfano jana tu wametengeneza nukuu ya uongo ikinukuu mimi Msemaji Mkuu wa Serikali kwamba nimesema Mwandishi wa Habari atakayenukuu taarifa za chombo kimoja cha habari cha kimataifa na video za uchochezi, eti atashtakiwa kwa uhaini, sijasema maneno haya wametengeneza.
Wametengeneza nukuu nyingine ya uongo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan eti ameagiza Mwandishi wa Habari wa Nchi Jirani anayefanya kazi chombo kimoja cha kimataifa wakamatwe na kushtakiwa kwa uhaini.
Nawaomba Watanzania tukatae kuruhusu mambo haya. Mheshimiwa Rais ameshasema Serikali ipo tayari kusikiliza wote wenye madukuduku, wenye ushauri na wenye maswali. Yote yatapokelewa na yatafanyiwa kazi. Hakuna sababu ya kuharibu nchi.
Wengine wanakwenda kutengeneza uongo kuwa mifumo yetu ya malipo na akaunti za amana katika benki na taasisi za fedha sio salama. NI UONGO MTUPU na Upuuzwe.
Natamani Watanzania mtambue kuwa malengo ya watu hawa, kutengeneza chokochoko, kufanya uchochezi mitandaoni na kwenye vyombo vya habari, kutia hasira watu ili waharibu nchi yao na mengine ni KUANGUSHA UCHUMI WA TANZANIA, NI KUHARIBU BIASHARA ZETU, NI KUPUNGUZA WATALII ILI TUKOSE FEDHA na kibaya zaidi ni kutaka Tanzania iadhirike ili washindani wetu wa kibiashara wanufaike.
Ni muhimu kutambua hii ni vita ya uchumi, huku kwenye habari (kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni njia ya kupita tu). Na tukiruhusu mtego huu tutakaoathirika ni sisi Watanzania wote.
NAOMBA KURUDIA kama nilivyosema awali, matukio yale yalitokea kwa siku chache na katika miji michache ya nchi yetu. Kwa sasa hali ni shwari na Watanzania wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea kuhakikisha watu na mali zao wanabaki kuwa salama na matishio yote ya kiusalama yanakabiliwa ipasavyo.
Shughuli zetu za kiuchumi zinaendelea vizuri na Tanzania kwa hivi sasa ni moja ya nchi chache ambazo zinakwenda kupiga hatua kubwa za kiuchumi kupitia miradi mikubwa na ya kimkakati inayoendelea na mingine imeanza kukamilika na kutoa huduma
Miradi kama;
SGR-Kazi inaendelea vizuri sana, kwa vipande vyote nane vya kuanzia Makutupora – Tabora, Tabora – Isaka, Isaka – Mwanza, Tabora – Kigoma na Kigoma kwenda Burundi.
Sasa hivi tupo katika maandalizi ya ujenzi wa reli mpya (tunakwenda kujenga njia ya Kaskazini {Tanga-Arusha-Musoma kilometa 1,028), njia ya Kusini {Mtwara -Mbambabay kilometa 1,000}.
Pia tunakamilisha maandalizi ya kuanza ujenzi wa treni za mjini zitakazopita juu katika Majiji yetu tukianza na Jiji la Dar es Salaam {zijulikanazo kama Mono Rail}tumepanga kuanza na Kawe, Mwenge, Mlimani City, Ubungo, kisha tunaelekea Kariakoo na kuunganisha na SGR.
Tutakuwa na tawi jingine la Bibi Titi kwenda Morocco kupitia barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kisha tunaunganisha Mwenge. Hii awamu ya kwanza na kila kilometa 2 tutaweka Kituo. Lengo tujenge mtandao wa kilometa 160.
Tutakuwa na treni hizi za Mjini pia katika Jiji la Dodoma ambapo tumepanga kujenga kuanzia stesheni ya SGR kwenda Mjini, kisha tutaunganisha kwenda Mtumba hadi Chamwino kupitia Stendi ya Mabasi.
Awamu ya pili tutaelekea Msalato Airport. Lengo kwa Dodoma tujenge kilometa Mtandao wa kilometa 105.
Uboreshaji wa Bandari yetu ya Dar es Salaam na jinsi tulivyojipanga kufikia nchi Jirani za Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Uganda, Zambia, Malawi.
Wote mmeona ufanisi katika bandari yetu ya Dar es Salaam umeongezeka maradufu na kuwa tishio kubwa kwa washindani wetu hasa baada ya Serikali kuamua kushirikiana na DP World ambapo sasa uwezo wa bandari kuhudumia mizigo umeongezeka maradufu kutoka kuhudumia tani Milioni 21 mpaka tani Milioni 32 ndani ya miaka 3 mapato ya bandari pia yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 900 hadi zaidi ya shilingi Trilioni 1.8 hivi sasa.
Meli zinashusha kwa haraka zaidi (muda wa meli kusubiri umepungua kutoka siku 46 hadi 7) na gharama za uendeshaji wa bandari zimeshuka na tunaokoa zaidi ya shilingi Bilioni 400 ikilinganishwa na kabla ya DP World.
Na mengine mengi mfano wote juzi tu tumeshusha meli ya 1 kati ya meli 4 tunazojenga katika ziwa Tanganyika {Hizi zinakwenda kuongeza biashara kubwa kati ya Tanzania na Kongo – mzigo uliokuwa unazunguka kupitia nchi Jirani utakuwa unatoka Tanzania kwenda Kongo moja kwa moja.
Tumejipanga hadi mwaka 2029 tufikie kuhudumia tani Milioni 50 ikilinganishwa na sasa tunahudumia tani Milioni 32 ambazo zimeongezeka kutoka kwenye matarajio ya tani Milioni 28.
Lakini pia tumefanya makubwa katika bandari zetu za Tanga na Mtwara. Kule Mtwara tunajenga bandari Kisiwa Mgao ambayo itahudumia mizigo yote iitwayo Dirty Cargo (Mfano Makaa ya Mawe, Saruji, Chuma, Klinka n.k).
Tanga tumeboresha bandari kwa kuongeza gati mbili na sasa meli nyingi zinapita Tanga, hata zile zilizokuwa zinapita bandari Jirani sasa zinapita Tanga.
Tulikuwa tunahudumia tani laki 4 na sasa tunahudumia tani Milioni 1.5 (Mwaka huu tutafika tani Milioni 2).
Uwezo wa Bandari yetu ya Tanga sasa ni tani Milioni 3 kwa mwaka. Na tunajenga gati nyingine 3 na kituo cha kupokelea mafuta
Halikadhalika tumekamilisha bandari ya Bukoba na Kemondo. Bandari ya Mwanza North nayo tunaikamilisha manaake mzigo wa Uganda utapita Tanzania (sasa hivi tunahudumia asilimia 3 tu, baada ya hapo tutaongeza hadi asilimia 38)
Bandari ya Bagamoyo, tunaanza kujenga Desemba hii 2025. Mitandao ya ujenzi ipo njiani na bandari hii itakuwa na kina cha hadi mita 20 na itakuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa kuliko bandari za ukanda huu wa mashariki. Tutajenga gati 28 (tutaanza na gati 14).
Bandari itakuwa na uwezo wa kuchukua meli zenye uwezo wa kubeba makontena hadi 25,000. TUJIULIZE NANI ATAKAYEPENDA?
Pia tumeanza kujenga Bandari ya Kigoma na mkandarasi yupo Site. Tutaongeza uwezo wake mpaka kufikia tani milioni 3 ikilinganishwa na sasa ambapo inahudumia tani laki 6.
Na mkumbuke miradi hii yote inakwenda kuajiri vijana wetu kwa maelfu na watapata kipato kizuri. Na tunajipanga kumwaga ajira kama mchele.
Kwenye utalii ndio usiseme, tuliweka lengo la kuongeza Watalii kufikia Milioni 5 hadi mwaka 2025, tumefanikiwa kuongeza hadi zaidi ya Watalii 5.3.
Na sasa tumeanza safari ya kufikia Watalii Milioni 8. Watalii hawa wanapoongezeka kwetu maana yake wanapungua kwa washindani wetu.
Shirika letu la ndege (ATCL) limeimarika sana. Sasa hivi tuna ndege 16 na kati ya sasa na 2030 tunakwenda kununua ndege zingine 8.
Sasa hivi tunahudumia vituo 29, kabla ya mwisho wa mwaka huu tunaongeza vingine 3 ambavyo ni Cape Town (Afrika Kusini), Accra (Ghana) na Victoria Falls (Zimbabwe). Hadi mwaka 2030 tutafika vituo 50 vya ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wa abiria sasa hivi tunahudumia abiria 1,500,000 na tunapanga kufika abiria 3,000,000 katika miaka miwili ijayo. Miaka minne iliyopita tulikuwa tunasafirisha abiria kama 800,000 tu kwa mwaka.
Uchumi wetu halikadhalika, unakuwa vizuri. Mwaka huu tunapanga ukue kufikia wastani wa asilimia 6.
Ni vizuri Watanzania wajue kuwa mafanikio haya ya bandari yanawaathiri washindani wetu, na kwa hiyo HATUWEZI KUPENDWA, TUTASHAMBULIWA TU.
Na tunaposhambuliwa namna hii, tunakwenda kuathiriki kama nchi na pia kwa mtu mmoja mmoja. Bandari zikiathirika tutakosa mapato, tutashindwa kununua dawa, kujenga barabara, kusambaza maji, kusambaza umeme kugharamia elimu, afya na mengine.
Utalii ukianguka na sisi wananchi tutakosa ajira, Mama lishe watakosa biashara, madereva wa taxi wataathirika na ajira zitapotea.
TUAMKE WATANZANIA
Kwa watalii (To our prestigious tourists), these are the few words from the government;
Welcome to the United Republic of Tanzania. Our nation remains peaceful, calm, and open to all who wish to explore its beauty—from Kilimanjaro and the Serengeti to Ngorongoro, Dar es Salaam, and Zanzibar to mention a few.
Please ignore any misinformation meant to distract you from the unforgettable experiences awaiting you here.
Our destinations are safe, our accommodations are improving every day, and our hospitality and transportation ensure that your journey is comfortable and memorable.
The government is fully committed to protecting you, your companions, and the value of your dollars and shilings while visiting our country.
Mwisho, jana nilitoa tangazo kwa umma baada ya chombo cha habari cha CNN kuchapisha makala ya matukio ya tarehe 29 Oktoba, 2025.
Kwanza uhakiki wa maudhui yaliyomo katika makala ile unaendelea lakini kama ambavyo chombo hiki kimefanya katika ripoti zake mbalimbali kimeendelea kufanya makosa ya kiweledi na kiuadilifu katika uandishi wa habari kwa kutangaza na kuchapisha maudhui ambayo yanaegemea upande mmoja.
Sio kweli kwamba CNN ilishindwa kupata upande wa Serikali kwa ripoti zao zote wanazotoa.
Inashangaza kwa chombo cha habari cha kimataifa kama CNN kufanya makosa makubwa ya kimaadili kama haya ambayo yamefanywa.
Serikali inatoa wito kwa CNN kuzingatia maadili na weledi katika uandishi wa habari na kujiepusha na uchapishaji wa taarifa zisizokuwa na vyanzo halali na rasmi, kupotosha na kuzua taharuki.
Najua mwandishi wa habari wa CNN aliyeandaa makala ile hakuwa Tanzania na ameandaa makala kwa kutumiwa picha zilizopigwa kwa simu wakati wa vurugu na bila kuwasiliana na mamlaka zinazohusika Tanzania amekwenda kuandaa makala ya upande mmoja.
Tusingependa tufikie kuwapa majina ambayo baadhi ya waliowakwaza wamewapa, waje tuwape upande wa Serikali na wakachapishe taarifa zenye usawa, ukweli na zisizo na mgongano wa kimaslahi.
Waache kuchagua kuripoti upande mmoja wakati upande mwingine upo na haujawanyima taarifa.
Baada ya kusema hayo naomba kurudia kuwahakikishia Watanzania na watu wote Dunia kuwa Tanzania ni salama, Tanzania imetulia, watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na yalitokea wakati wa Uchaguzi Mkuu yanachunguzwa na matokeo yake yatafanyiwa kazi.
Waandishi wa Habari wenzangu tuendelee kuilinda nchi yetu kwa wivu mkubwa, maendeleo tunayopata sasa wapo ambao yanawakwaza na watatafuta kila njia ya kutuangusha TUKATAE.






