SAMARKAND-Nyota ya Kiswahili imeendelea kuangaza Kimataifa baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuridhia Lugha hiyo kuwa moja ya Lugha zitakazotumika Rasmi katika Mikutano Mikuu ya Shirika hilo.
Kauli hiyo imetolewa katika Mkutano Mkuu wa 43 wa Shirika hilo uliofanyika Samarkand nchini Uzbekistan kuanzia tarehe 30 Oktoba na unaotarajiwa kuhitimishwa Novemba 13 mwaka 2025.
Tamko hilo la UNESCO ambalo limetolewa Novemba 11, 2025, limetokana na maombi yaliyowasilishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kupitia wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Kwa kushirikiana na Mabaraza ya Kiswahili Tanzania BAKITA na BAKIZA.
Kufuatia hatua hiyo, tayari Tanzania imepewa fursa ya kuwasilisha hotuba ya nchi baada ya maombi yake kuridhiwa. hotuba ambayo imetolewa na Mhe. Ali Jabiri Mwadini, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na mwakilishi wa kudumu wa UNESCO.
Kupitishwa kwa Kiswahili kuwa Lugha ya kazi kunafanya Lugha hiyo kuwa ya kwanza yenye asili ya Afrika kupewa hadhi hiyo huku hatua hii muhimu ikitarajiwa kufungua milango mingi zaidi ya Kiswahili katika taasisi, mashirika ya Umoja wa Kikanda na Kimataifa.
Aidha, ikumbukwe kuwa, UNESCO Katika Mkutano wake wa 41 wa Novemba 2021 ndio uliopitisha azimio la kuwa na Siku ya Kiswahili Duniani ambayo huadhimishwa Julai 07 ya Kila Mwaka na siku hiyo ilitambuliwa rasmi na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Julai, 2024.
Kiswahili kwa sasa ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Wazalishaji Almasi Afrika (ADPA) na Umoja wa Afrika (AU).Nafasi hizi za Kiswahili Kimataifa zinatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha ajira na fursa kwa wataalamu wa Kiswahili katika Ufundishaji, Tafsiri, Ukalimani, Uandishi wa Vitabu na Utangazaji.




