NA DIRAMAKINI
YOUNG Africans Sports Club (Yanga SC) imeibuka na ushindi wa kishindo wa mabao 4-1 dhidi ya KMC FC FC katika mtanage wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Ushindi huo mnono wameupata leo Novemba 9,2025 katika dimba la KMC Complex lililopo Mwenge katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katika mtanage huo,Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 36 alifungua pazia la mabao, ingawa Darueshi Saliboko dakika ya 45 alisawazisha. Pacome Zouzoua alirejea nyavuni dakika ya 74 kulipa bili.
Aidha,Andy Boyeli alitupia bao la tatu kwa penalti huku akirejea tena dakika ya 90' kufunga hesabu kwa bao la nne.
Kwa matokeo hayo Young Africans Sports Club (Yanga SC) imejikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo kwa kufikisha alama 10.
Nafasi ya pili inashikiliwa na watani zao Simba Sports Club (Simba Simba SC) kwa alama tisa baada ya mechi tatu, huku Yanga ikiwa tayari imecheza mechi nne.
Aidha, Pamba Jiji FC inaendelea kuwa nafasi ya tatu kwa alama tisa baada ya mechi sita, nafasi ya nne inashikiliwa na Mbeya City FC kwa alama nane baada ya mechi sita.
Kwa upande wa nafasi ya tano inashikiliwa na Mashujaa FC kwa alama nane baada ya mechi sita, huku KMC FC ikiburuza mkia kwa alama tatu baada ya mechi sita.
