Askari waliotimiza miaka 12 kazini wafanya matendo ya huruma

RUVUMA-Askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma waliotimiza miaka 12 kazini wamefanya matendo ya huruma kwa kutembelea na kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto yatima cha SWACCO kilichopo Kata ya Mkuzo Manispaa ya Songea.

Huo ni moja ya mchango wao wa kuwafariji watoto wa kituo hicho pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwalinda kipindi chote cha miaka hiyo kazini.
Akizungumza kwa niaba ya askari wenzake Mkaguzi wa Polisi (INSP),Godson Mbuya amesema kuwa,umoja wao wa askari wa H2 mkoani Ruvuma wameona ni vyema kutembelea kituoni hapo ili waweze kutoa msaada wa kidogo walichojaaliwa.

Ni msaada ambao umeenda sambamba na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwalinda kipindi chote cha miaka kumi na mbili kazini.
Naye INSP Daud Asulwisye amebainisha kuwa, Jeshi la Polisi limekuwa na utamaduni wa kutembelea vituo vya watoto wenye uhitaji na kutoa misaada mbalimbali kwa makundi yenye uhitaji.

Aidha,amewaomba watu wengine kutoka taasisi binafsi, wafanyabiashara na wale wote ambao watajaaliwa chochote waweze kutembelea vituo vyenye uhitaji vya kulelea watoto yatima ili waweze kuwafariji watoto hao ili nao waweze kufarijika na kujiona wapo sawa na watoto wengine.
Kwa upande wa Meneja Mradi wa Kituo cha SWACCO, John Kinguku amelishukuru Jeshi la Polisi kwa mchango mkubwa wa kuendelea kutambua uhitaji wa kituo hicho na kuwa na mchango mkubwa wa kutembelea kituoni hapo na kuwapatia mahitaji mbalimbali watoto wenye uhitaji.

Amesema kuwa, vitu hivyo vitaenda kuwa msaada mkubwa kwa watoto hao hasa kipindi cha kuelekea sikukuu ya Christmas.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news