DAR-Uongozi wa DIRAMAKINI leo Desemba 23,2025 unaungana na wananchi wote wa Zanzibar pamoja na Watanzania kwa ujumla kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuiongoza Zanzibar kuelekea maendeleo, umoja na ustawi wa wananchi.


Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa DIRAMAKINI, Godfrey Ismaely Nnko leo ameeleza kuwa, siku hii ni fursa adhimu ya kutafakari na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt.Mwinyi tangu alipoingia madarakani, ambapo ameonesha uongozi wenye dira, uwajibikaji na kujali maslahi mapana ya wananchi.
Aidha,uongozi wa DIRAMAKINI umepongeza juhudi za Rais Dkt. Mwinyi katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar kupitia sera na mikakati mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kukuza uchumi wa buluu, kuvutia uwekezaji wa ndani na nje, pamoja na kuimarisha mazingira bora ya biashara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,hatua hizo zimechangia kuongeza fursa za ajira, kuinua kipato cha wananchi na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Pia, Rais Dkt.Mwinyi ameendelea kuonesha dhamira ya dhati katika kuboresha huduma za kijamii, hususan katika sekta za elimu na afya.
Vilevile, Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wake imeendelea kuboresha miundombinu ya shule na hospitali, kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, na kuweka mazingira rafiki kwa maendeleo ya rasilimali watu, jambo linaloonesha kujali ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.
Katika eneo la miundombinu, uongozi wa DIRAMAKINI umeeleza kuridhishwa na juhudi zinazoendelea kufanyika katika ujenzi na ukarabati wa barabara, bandari, viwanja vya ndege pamoja na miradi mingine ya kimkakati inayolenga kuimarisha usafiri na mawasiliano.
Miradi hiyo imekuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
Uongozi huo pia umepongeza mchango wa Rais Dkt. Mwinyi katika kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa wananchi.
Kupitia uongozi wake wa busara na ushirikishwaji, Rais Dkt.Mwinyi ameendelea kuhimiza umoja, maridhiano na mshikamano wa kitaifa, misingi ambayo ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
DIRAMAKINI imesisitiza kuwa, uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi umeendelea kujengwa juu ya misingi ya uwazi, usikivu na utawala bora, hali inayoongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao na kuimarisha demokrasia.
Kwa kutambua mafanikio hayo, uongozi wa DIRAMAKINI umemtakia Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi afya njema, maisha marefu, nguvu na hekima zaidi ili aendelee kuliongoza taifa kwa weledi na mafanikio makubwa zaidi.
Vilevile, umeendelea kuwasihi wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga Zanzibar yenye maendeleo, amani na ustawi kwa wote.