NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuwa,mifumo ya hali ya hewa iliyopo kwa sasa inaonesha kuendelea kuimarika kwa Ukanda Mvua na hivyo kuendelea kusababisha vipindi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa nchini.
Miongoni mwa mikoa hiyo ni Arusha,Manyara, Kilimanjaro, Mara, Simiyu, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa siku ya kesho Desemba 29,2025.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 28,2025 na TMA ikiangazia mwenendo wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
"Mnamo tarehe 26 hadi 27 Desemba, 2025 mamlaka iliendelea kutoa tahadhari ya vipindi vya mvua kubwa katika maeneo mengi nchini kuanzia tarehe 26 hadi 29 Desemba,2025."
Kwa mujibu wa tahadhari hiyo maeneo yaliyotarajiwa kuathirika na vipindi hivi vya mvua kubwa ni pamoja na mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe,
Mingine ni Dodoma, Singida, Songea, Morogoro, Lindi, Mtwara, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumisha Kisiwa cha Mafia) pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba.
"Kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi hivi sasa maeneo mengi nchini yameendelea kupata vipindi vya mvua kubwa zikiambatana na upepo mkali na hivyo kusababisha uharibifu wa mali na miundombinu katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
"Hadi kufikia saa 3:00 kamili asubuhi ya leo viwango vya mvua kubwa vinavyozidi milimita 50 ndani ya saa 24 vilipimwa katika vituo vya Same (milimita 94.5), Morogoro (milimita 58.6) na Tabora (milimita 55.4)."
Aidha, viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine ni pamoja na Hombolo (milimita 49.5), Kibaha (milimita 43.6), Dodoma (milimita 36.6) na Iringa (milimita 35.6).
"Hadi muda huu tumepokea taarifa kuwa mvua hizo zimesababisha athari katika miundombinu ya reli ya zamani ya MGR kwa kuathiri madajara katika eneo la Kidete, Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro na Gulwe Wilaya Dodoma; kusababisha hitilafu za umeme wa TANESCO pamoja na umeme wa SGR.
Sambamba na Barabara Kuu ya Morogoro - Iringa eneo la Mama Marashi-Mikumi kumetokea maporomoko ya mawe na tope kurundikana barabarani.
"Mvua hizo zimesababisha miundombinu na shughuli za usafiri wa abiria na shehena kwa ujumla kuathirika, hususan kupitia Reli ya SGR.Kwa ujumla Serikali inaendelea na juhudi za kurejesha hali hiyo katika hali yake ya kawaida."
TMA imewashauri wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka mamlaka hiyo pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Mvua Kubwa
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
