Waziri Pembe asisitiza umuhimu wa michezo SUZA kampasi ya Benjamin Mkapa kisiwani Pemba

ZANZIBAR-Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Riziki Pembe Juma ameutaka Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Kampasi ya Benjamin Mkapa Pemba, kuandaa timu za mpira wa miguu kutoka ndani ya jamii inayowazunguka ili ziweze kushiriki na kushindana katika Bonanza la Michezo la chuo hicho, hatua inayolenga kukuza uhusiano mwema kati ya chuo na jamii.
Dkt. Riziki, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkusanyiko wa Kitaaluma (Convocation) wa SUZA, ameyasema hayo wakati wa Bonanza la Michezo na Utamaduni lililofanyika katika viwanja vya Mchangamdogo, Pemba.

Amesema,michezo ni chombo muhimu kinachoimarisha afya, upendo na mshikamano miongoni mwa washiriki, na kwamba ushirikishwaji wa timu za kijamii utaongeza mashirikiano mazuri kati ya chuo na jamii husika.
Aidha, ameuagiza uongozi wa chuo hicho kulifanya bonanza hilo kuwa la mara kwa mara kila muhula wa masomo unapokamilika, ili kuwasaidia wanafunzi kujenga afya ya akili na kimwili, badala ya kusubiri kumalizika kwa mwaka mzima wa masomo.

Vilevile, amehimiza kuendelezwa kwa michezo ya asili ikiwemo kukuna nazi, kusuka makuti, pakacha na michezo mingine ya kimila, kwa lengo la kudumisha na kukuza utamaduni wa Kizanzibari.

Hata hivyo, amewataka wanafunzi na wanajamii kuendelea kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano uliopo kati yao na chuo hicho, akisisitiza kuwa mazingira hayo ni msingi wa kufanikisha malengo ya kutoa elimu bora kwa watoto wao.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Abdi Talib Abdallah, amesema lengo la kuanzishwa kwa bonanza hilo ni kukuza vipaji vya wanafunzi wa chuo hicho katika nyanja mbalimbali za michezo na utamaduni.

Aidha, ameahidi kuyafanyia kazi maagizo yote aliyoyapokea kwa maslahi ya wanafunzi, chuo na taifa kwa ujumla.
Katika bonanza hilo, kulifanyika michezo mbalimbali ya kimila na kisasa ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, mbio za magunia, kula matikiti, kufukuza kuku na kusuka makuti, ambapo washindi walikabidhiwa zawadi mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news