Hatiani kwa tuhuma za mauaji Morogoro

MOROGORO-Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Rashid Hussein Paulo (35), mkulima na mkazi wa Msowelo, kwa tuhuma za kumuua Steven Elia Mayungu (26), mkulima na mkazi wa Mayungu, katika tukio lililotokea Desemba 26,2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi, tukio hilo lilitokea majira ya saa 5:00 usiku katika Kitongoji cha Shuleni, Kijiji na Kata ya Lumuma, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.

Uchunguzi wa awali unaeleza kuwa kulizuka ugomvi kati ya watu hao wawili, ambapo mtuhumiwa anadaiwa kumchoma marehemu kwa kitu chenye ncha kali eneo la kifuani, na kusababisha kifo chake.

Inadaiwa kuwa chanzo cha ugomvi huo kilihusishwa na wivu wa kimapenzi. Jeshi la Polisi limeeleza kuwa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa ajili ya mahojiano zaidi huku taratibu za kisheria zikiendelea, kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha jeshi la polisi linatoa wito kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mikononi na badala yake kutumia vyombo vya dola na mamlaka husika kutatua migogoro ya kifamilia au kijamii kwa njia ya amani na kwa kufuata sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news