DAR-Nassor Idrissa (Father) amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya kupata kura saba (7) dhidi ya kura sita (6) za mpinzani wake CPA Hosea Lugano kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 29, 2025 katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar Es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Nassor alisisitiza chini ya utawala wake atahakikisha haki inapatikana kwa kila timu bila kujali ukubwa wa timu, hususani maamuzi yanayotolewa ndani ya dakika 90 za mchezo.
Katika hatua nyingine,Hassan Muhsini Mwenyekiti wa Coastal Union amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ambapo katika nafasi hiyo hakuwa na mpinzani, hivyo kupitishwa kwa kura ya ndio wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Pia,Japhet Makau Rais wa Fountain Gate na Gilbert Nkolonko Mwenyekiti wa Mbeya City wamechaguliwa kuwa wajumbe wawakilishi wa klabu za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Aidha, Ahmed Gao wa Bigman na John Ndumbaro wa Mbeya City wamechaguliwa kuwa wajumbe wawakilishi wa klabu za Ligi ya Championship ya NBC wakati huo huo Azim Khan wa Dar City amechaguliwa kuwa mjumbe mwakilishi wa klabu za First League.













