ARUSHA-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linashiriki katika Kongamano la 16 la Mwaka la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi jijini Arusha.
Aidha,kongamano hilo linawakutanisha pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya ununuzi na ugavi.
Katika kongamano hilo, NHC ni miongoni mwa wadhamini, jambo linalodhihirisha dhamira ya shirika hilo katika kuunga mkono maendeleo ya taaluma ya ununuzi na usimamizi wa mnyororo wa ugavi nchini.
Ushiriki wa NHC katika mikutano na makongamano ya kitaaluma kama hili umeendelea kuleta matokeo chanya katika kuimarisha sekta ya makazi nchini.
Kupitia majukwaa haya, NHC hupata fursa ya kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za usimamizi wa ununuzi na ugavi, hali inayochangia kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya nyumba, kupunguza gharama, na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Vilevile, makongamano haya huchochea ubunifu, matumizi ya teknolojia za kisasa, pamoja na uimarishaji wa uongozi katika usimamizi wa rasilimali, mambo ambayo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za ongezeko la mahitaji ya makazi nchini.
Ushiriki wa NHC pia huimarisha ushirikiano na wadau wa sekta binafsi na taasisi za kitaaluma, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo endelevu ya sekta ya makazi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.