MANAMA-Tanzania imeendelea kushikilia nafasi yake ya kimataifa kama “Nchi Inayoongoza Duniani kwa Utalii wa Safari” katika Hafla ya Fainali za World Travell Awads 2025.

Tanzania imetunukiwa taji hili adhimu katika Sekta ya utalii duniani wakati wa Hafla ya 32 ya World Travel Awards (WTA 2025), iliyofanyika katika Ukumbi wa Exhibition World Center nchini Bahrain tarehe 6 Desemba 2025.
Tuzo za WTA, zinazotajwa kama “Tuzo za Oscars za utalii duniani” kutokana na hadhi yake kubwa katika Sekta, Tuzo hizi zimewaleta pamoja zaidi ya washiriki 500 wakiwemo viongozi wa Serikali na wadau wa utalii.
Tanzania imeshinda tuzo nne ikiwemo ya Kisiwa mashuhuri cha Zanzibar (Spice Islands) kushinda Tuzo ya World MICE Awards 2025 kama “Eneo Bora Afrika kwa Mikutano na Matukio ya Kitaasisi.”
Halikadhalika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, imetangazwa kuwa “Hifadhi Bora ya Taifa Duniani 2025” katika tuzo hizo za WTA.
Aidha, Tanzania imepata tuzo mbili zaidi katika kundi la Sekta Binafsi, ikiwemo “Kampuni Bora ya Safari za Puto Duniani,” iliyotwaliwa na kampuni ya Serengeti Balloon Safaris.
Tuzo nyingine imekwenda kwenye Kisiwa bora cha Mapumziko Duniani na Jumaira Thanda Resort katika Kisiwa cha Mafia nchini Tanzania imeibuka mshindi katika kipengele hicho.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo za WTA, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema tuzo hizo ni uthibitisho wa kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Tanzania pamoja na sekta binafsi katika kukuza utalii endelevu na kuimarisha uhifadhi nchini.Tanzania, ambayo imeshinda tuzo kwa mwaka wa pili mfululizo, inatarajiwa kuwa mwenyeji wa hafla ya fainali ya World Travel Awards itakayofanyika Desemba 2026.
Tags
Habari
Kimataifa
Sekta ya Utalii Tanzania
Tuzo Sekta ya Utalii
Viongozi wa Maliasili na Utalii Tanzania
Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania
World Travel Awards





