NA DIRAMAKINI
KATIKA kipindi cha Desemba Mosi hadi 10,2025 migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo kaskazini mwa dunia (Azore na Siberia) iliendelea kuimarika wakati ile iliyopo kusini mwa dunia (St. Helena na Mascarene)
iliendelea kudhoofika.
Hayo ni kwa mujibu wa muhtasari wa mwenendo wa mvua kwa siku 10 zilizopita na matarajio kwa siku 10 zijazo uliotolewa leo Desemba 10,2025 na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
TMA imebainisha kuwa,hali hii ilisababisha sehemu ya ukandamvua (ITCZ) kusogea kuelekea kusini na kuwepo katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, magharibi mwa nchi, nyanda za juu kusinimagharibi na maeneo jirani, hali ambayo iliimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo.
Vilevile, uwepo wa upepo wenye unyevunyevu
uvumao kutoka baharini kuelekea maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi yetu uliimarisha
mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo hasa katika kipindi cha siku tano za
mwisho
"Viashiria vilivyotajwa hapo juu vilipelekea uwepo wa vipindi vya mvua zilizoambatana na
ngurumo za radi katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, magharibi mwa nchi na nyanda za juu kusini magharibi."
Pia, vipindi vya mvua katika maeneo machache ya ukanda wa pwani na nyanda za juu kaskazini mashariki.
Katika kipindi hiki, migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo kaskazini mwa dunia (Azore na
Siberia) inatarajiwa kuendelea kuimarika wakati ile iliyopo kusini mwa dunia (St. Helena na Mascarene) inatarajiwa kuendelea kudhoofika.
Hali hii inatarajiwa kusababisha sehemu ya ukandamvua (ITCZ) kusogea kuelekea kusini na kuwepo katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, magharibi mwa nchi, kati, nyanda za juu kusinimagharibi na kusini mwa nchi, hali ambayo inatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo.
Vile vile, uwepo wa upepo wenye unyevunyevu uvumao kutoka baharini kuelekea maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi yetu unatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo.
Kuhusu mwelekeo wa mvua kwa Desemba 11 hadi 20,2025 TMA imefafanua kuwa,Kanda ya ziwa Victoria inayojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara) mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache.
Aidha,Nyanda za juu kaskazini-mashariki inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.
Pwani ya kaskazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.
Magharibi mwa nchi inayojumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache.
Kanda ya kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma na Singida mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.
Nyanda za juu Kusini-magharibi inayojumuisha mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache.
Aidha,Pwani ya kusini inayojumuisha mikoa ya Mtwara na Lindi mvua zinatarajiwa katika maeneo machache na kanda ya kusini inayojumuisha mikoa wa Ruvuma na maeneo ya kusini mwa Morogoro mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
