NA DIRAMAKINI
SERIKALI imesema kuwa, kila mtahiniwa aliyefanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwaka, 2025 na kupata jumla ya alama za ufaulu kati ya 121 hadi 300 amechaguliwa na kupangiwa shule ya Serikali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameyasema hayo leo Desemba 4,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Waziri alikuwa akielezea kuhusu kukamilika kwa zoezi la Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Kwanza (K1) kwa mwaka wa masomo wa 2026.
"Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM TAMISEMI) imekamilisha zoezi la Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Kwanza (K1) kwa mwaka wa masomo wa 2026 kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia."
Profesa Shemdoe amesema,uchaguzi huu umehusisha wanafunzi 937,581 sawa na asilimia 100 ya wanafunzi wote waliokuwa na sifa ya kuchaguliwa.
Idadi hiyo inajumuisha wasichana 508,477 na wavulana 429,104 ambapo wanafunzi hao ni wale waliofanya na kufaulu Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi mwaka, 2025.
Amesema,uchaguzi wa wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka wa masomo, 2026 umezingatia kigezo cha ufaulu wa mtahiniwa anayechaguliwa.
Waziri huyo amesema,Shule za Sekondari za Bweni za Serikali zimegawanyika katika makundi matatu ambayo ni Shule za Sekondari za Bweni za Wanafunzi wenye ufaulu wa Juu (Special Schools), Shule za Sekondari za bweni za Amali na Shule za bweni za Kitaifa.
"Shule za Sekondari za bweni ni za Kitaifa hivyo, zimepangiwa wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa kuzingatia mgawanyo wa nafasi uliobainishwa na vigezo vilivyowekwa ili kuimarisha Utaifa."
Uchaguzi wa wanafunzi katika makundi hayo ulifanyika kwa mujibu wa Mwongozo wa Uchaguzi wa mwaka 2024 kama ifuatavyo:
Shule za Sekondari za Bweni kwa Wanafunzi wenye Ufaulu wa Juu Nafasi katika shule za wanafunzi wenye Ufaulu wa Juu zimegawanywa kwa kila Mkoa kulingana na idadi ya watahiniwa wa Darasa la Saba waliotahiniwa katika Mkoa husika kwa kutumia Kanuni ya kugawa nafasi hizo Kitaifa.
Aidha,nafasi zilizotolewa kwa Mkoa zimegawanywa sawa kwa Halmashauri zote bila kujali idadi ya watahiniwa waliotahiniwa katika Halmashauri.
Nafasi katika Shule za Sekondari za Amali, amesema zimegawanywa kwa kila Mkoa kulingana na idadi ya watahiniwa wa Darasa la Saba kwa Mkoa husika kwa kutumia Kanuni ya kugawa nafasi hizo Kitaifa.
Amesema,nafasi zilizotolewa kwa Mkoa zimegawanywa sawa kwa kila halmashauri bila kujali idadi ya watahiniwa waliotahiniwa katika halmashauri.
"Nafasi katika Shule za Bweni za Kitaifa zimegawanywa kwa kila halmashauri kwa kufuata idadi ya watahiniwa wa Darasa la Saba waliotoka katika halmashauri husika kwa kutumia Kanuni ya kugawa nafasi hizo Kitaifa.
"Jumla ya wanafunzi 937,581 wakiwemo wasichana 508,477 na wavulana 429,104 ikijumuisha wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 3,228 wakiwemo wasichana 1,544 na wavulana 1,684 wamepangwa katika shule za sekondari za Serikali 5,230 kwa ajili ya kuanza masomo ya Kidato cha Kwanza mwaka, 2026 kwa mgawanyo ufuatao:-
"Jumla ya wanafunzi 815 wakiwemo wasichana 335 na wavulana 480 wamechaguliwa kujiunga katika shule za sekondari ambazo hupokea wanafunzi wenye ufaulu wa Alama za Juu. Shule hizo ni Ilboru, Msalato, Kibaha, Kilakala, Mzumbe, Tabora Boys na Tabora Girls."
Pia, amesema jumla ya wanafunzi 3,441 wakiwemo wasichana 1,279 na wavulana 2,162 wamechaguliwa kujiunga na Shule za Amali Bweni.
Aidha,jumla ya Wanafunzi 7,360 wakiwemo wasichana 5,014 na wavulana 2,346 wamechaguliwa kujiunga na Shule za Bweni za Kitaifa.
"Jumla ya wanafunzi 925,965 wakiwemo wasichana 501,849 na wavulana 424,116 wamechaguliwa kujiunga katika shule za sekondari za Kutwa ambazo hupokea wanafunzi kutoka katika eneo la karibu na shule ya msingi aliyosoma mwanafunzi husika."
Waziri Shemdoe amesema,Serikali ilifanya maandalizi mapema ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaofaulu Mtihani wa kumaliza Darasa la Saba mwaka, 2025 wanajiunga na Elimu ya Sekondari ifikapo Januari, 2026.
"Kutokana na maandalizi hayo Wanafunzi wote 937,581 wakiwemo wasichana 508,477 na wavulana 429,104 waliofaulu Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi 2025 wataanza muhula wa kwanza wa masomo wa mwaka 2026 utakaoanza tarehe 13 Januari, 2026.
"Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka, 2026."
"Vilevile, nawashukuru Viongozi wa ngazi ya Mkoa, Wilaya, Halmashauri, Wakuu wa Shule, Walimu na Wadau wa Elimu nchini kwa kutoa ushirikiano katika kusimamia uendeshaji na utoaji wa Elimu ya Msingi na Sekondari nchini.
"Aidha, napenda kuwaasa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2026 nchini watumie vizuri fursa waliyoipata kusoma kwa bidii ili wafikie malengo waliojiwekea na matarajio ya wazazi."
BOFYA JINA LA SHULE KUONA ORODHA YA WANAFUNZI
Maelekezo ya Jumla ya Utekelezaji wa Mtaala Ulioboreshwa kuanzia Januari, 2026
"Kama mjuavyo, mnamo mwezi Januari, mwaka 2024 tulianza utekelezaji wa Mitaala iliyoboreshwa kwa Toleo la 2023 ya Elimu Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari. Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI inaendelea na utekelezaji wa mitaala hiyo.
"Hivyo, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinahimizwa kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa mitaala hiyo kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na ufanisi wa utekelezaji. Katika kuweza kutekeleza vema mitaala hiyo ninatoa maelekezo yafuatayo:
"Kila shule ya sekondari itumie vema kipindi cha orientation kwa wanafunzi kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuwasiliana katika lugha ya Kiingereza na kuchagua aina ya fani wanazopenda kusoma katika shule zenye mkondo wa amali zisizo za kihandishi;
"Wazazi/Walezi kufanya maandalizi ya kutosha kwa watoto waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka wa masomo 2026 ili kuepuka watoto kuchelewa kuanza masomo yao kwa wakati; na
"Mikoa na Halmashauri zote nchini zihakikishe wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka wa masomo 2026 wanaripoti shuleni na kuandikishwa ili kupata haki yao ya msingi ya elimu.
"Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi na Watendaji wa Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha Wanafunzi wote waliochaguliwa wanaanza masomo yao mwezi Januari, 2026 bila vikwazo vya aina yoyote ili kutekeleza azma ya Serikali ya utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo.
"Hivyo, ninawaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Shule kuhakikisha maandalizi yote kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka, 2026 yanakamilika kwa wakati ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni ifikapo tarehe 12 Januari, 2026 kwa wanafunzi waliochaguliwa Shule za Bweni na tarehe 13 Januari, 2026 kwa wanafunzi waliochaguliwa Shule za Kutwa.
"Vilevile, ninawahimiza, Wazazi, Walezi na Jamii kushirikiana na Uongozi wa Shule, Mikoa, Wilaya na Halmashauri ili kuhakikisha kuwa Wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa, wanahudhuria na kubakia Shuleni hadi watakapohitimu Elimu ya Sekondari."
OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA KWANZA, 2026
BOFYA HAPA KUONA ORODHA YA WANAFUNZI WALIOPANGWA KWENDA SHULE MOJA
CHAGUA MKOA ULIKOSOMA
| ARUSHA | DAR ES SALAAM | DODOMA |
| GEITA | IRINGA | KAGERA |
| KATAVI | KIGOMA | KILIMANJARO |
| LINDI | MANYARA | MARA |
| MBEYA | MOROGORO | MTWARA |
| MWANZA | NJOMBE | PWANI |
| RUKWA | RUVUMA | SHINYANGA |
| SIMIYU | SINGIDA | SONGWE |
| TABORA | TANGA |
.jpeg)