DODOMA-Katika nia ya kuhakikisha unyumbufu katika utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetangaza uamuzi wa kuwaondolea baadhi ya masomo wahitimu wa elimu ya juu wanaojiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA.
Uamuzi huo umetangazwa tarehe 23 Desemba 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore wakati akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi kwa ajili ya mwaka wa masomo unaoanza Januari 2026, katika ofisi za VETA Makao Makuu, jijini Dodoma.“Mwaka huu jumla ya waombaji 134 ni wahitimu wa Astashahada, Shahada, na Shahada ya Uzamili. Waliochaguliwa ni 123. Waombaji kwenye kundi hili wameondolewa masomo ambayo walishayasoma wakati wanajipatia elimu kulingana na taaluma zao,” amesema.
Amesema kundi hilo limepunguziwa masomo Bebezi kama Sayansi ya Uhandisi (Engineering Science) na Uchoraji wa Kihandisi (Technical Drawing) kwa wanaosoma stadi za kihandisi ambayo hulenga kumsaidia mwanachuo kupata maarifa ya fani husika, pamoja na Masomo Mtambuka kama Stadi za Maisha na Stadi za Mawasiliano ambayo kumuwezesha mwanachuo kumudu mazingira na ushindani mahala pa kazi.
“Kwa hiyo, kwa kuzingatia elimu za waombaji wenye elimu za juu, uchambuzi umefanyika na kuanisha masomo mtambuka au bebezi ambayo hawatajifunza kwa kuwa tayari wana maarifa na ujuzi wa masomo hayo. Kwa kufanya hivyo, kutawawezesha kuhitimu mapema zaidi, mathalani badala kujifunza stadi za Ngazi ya Kwanza na ya Pili kwa miaka miwili, watafanya kwa mwaka mmoja tu,” amesema.
CPA Kasore amesema uamuzi huo umefanyika kwa nia ya kuwezesha kundi hilo kuhitimu kwa muda mfupi zaidi na kuongeza idadi ya watanzania wenye ujuzi mahiri katika soko la ajira na kazi na kuweka motisha ya kujiunga na ufundi stadi.
Amesema,mwamko wa vijana wenye sifa za elimu mbalimbali kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi unaendelea kuongezeka na hivyo VETA inabuni afua mbalimbali ili kuwawezesha kuendelea kupata mafunzo bora na pasipo vikwazo.