ZANZIBAR-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Mheshimiwa Idrissa Kitwana Mustafa amesema, Serikali ya Awamu ya Nane imejikita katika kuwaletea maendeleo wananchi katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya michezo.
Mheshimiwa Kitwana ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Kiwanja cha Mpira wa Miguu cha Mwehe, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, hafla iliyofanyika ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.Amesema,ujenzi wa kiwanja hicho ni hatua muhimu katika kuboresha michezo na kukuza vipaji vya wananchi wa eneo hilo.
Ameeleza kuwa,Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yameleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wananchi, na kwamba Serikali iliyopo madarakani inaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo pamoja na kuibua vipaji mbalimbali kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi Zanzibar.
Aidha, amefahamisha kuwa kiwanja hicho kimejengwa kwa ubora wa hali ya juu na kinaweza kutumika kwa michezo mbalimbali ya ndani na nje, sambamba na shughuli nyingine za kijamii.
“Mapinduzi ya Zanzibar yamethibitisha kuwa kwa umoja na mshikamano tunaweza kufikia malengo yetu. Serikali inaendelea kuimarisha sekta ya michezo ili kuleta maendeleo kwa jamii yetu,” alisema Mheshimiwa Kitwana.
Sambamba na hayo, ameeleza kuwa ujenzi wa viwanja vya michezo ni sehemu ya utekelezaji wa dira na maono ya Serikali katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya michezo kwa manufaa ya wananchi wote.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Ndg. Mattar Zahour, amesema mradi huo ni muendelezo wa juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuimarisha sekta ya michezo kwa kuwapatia wananchi mazingira bora ya kukuza vipaji vyao.
Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu uwanja huo, Ndg. Zahour amesema mradi huo umegharimu jumla ya Dola za Kimarekani milioni 2.2 na ulitekelezwa chini ya Kampuni ya Uniform Sport ya Uturuki.