NA LWAGA MWAMBANDE
MARA nyingi wataalamu wa maendeleo ya jamii wanasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii ili kujenga maisha bora ya sasa na uzeeni.
Picha na Mtandao.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, juhudi na nidhamu katika kazi huwezesha mtu kujiandaa kiuchumi, kiafya na kijamii kwa siku zijazo.
Aidha,kufanya kazi kwa nguvu humsaidia mtu kupata kipato, kuweka akiba na kuwekeza, jambo linalopunguza changamoto za kifedha anapofikia uzee.
Pia, watu waliokuwa wachapa kazi huendelea kuwa na afya njema ya akili na heshima katika jamii hata wanapostaafu.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anahimiza kila mmoja kutumia vyema nguvu za ujana na utu uzima kwa kufanya kazi halali na kupanga maisha ya baadaye, kwani uzee wenye utulivu na heshima huanza na juhudi za leo.Endelea;
1. Wakati unazo nguvu, muda wa kuchakarika,
Utapoishiwa nguvu, muda wa kupumzika,
Hapa nawapa makavu, ambao mwazubaika,
Biashara asubuhi, Jioni ni mahesabu.
2. Ujana ni asubuhi, muda wa kuhangaika,
Kusanya kusanya wahi, uzee unainuka,
Kipata staftahi, kimbia kuwajibika,
Biashara asubuhi, jioni ni mahesabu.
3. Kijana wakaa kaa, kama mzee kachoka,
Uchumi lini tapaa, uweze kufurahika?
Wajiletea balaa, uzee ukikufika,
Biashara asubuhi, jioni ni mahesabu.
4. Wengi unaowaona, uzeeni wanemeka,
Walipokuwa vijana, kazi walishughulika,
Fursa waliziona, na hizo wakazidaka,
Biashara asubuhi, jioni ni mahesabu.
5. Pengine wasubiria, mirathi uje kushika,
Wazee ninakwambia, wapo hawataondoka,
Tabaki wajililia, fikira zilopotoka,
Biashara asubuhi, jioni ni mahesabu.
6. Utakaa unawaza, lini baba tatoweka,
Hapo unajimaliza, hataondoka haraka,
Na tena wajilemaza, uzee unakufika,
Biashara asubuhi, jioni ni mahesabu.
7. Kwa kweli inashangaza, wazee waneemeka,
Kama ukiwauliza, wanabakia kucheka,
Ujana walikoleza, kazi bila ya kuchoka,
Biashara asubuhi, jioni ni mahesabu.
8. Vya kurithi si vitamu, kama vya kuchakarika,
Wakati mwingine sumu, amani inatoweka,
Ukiweza kujikimu, hiyo ni bora hakika,
Biashara asubuhi, jioni ni mahesabu.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
