DAR-Daruwesh Ali bin Mussa Al-Maaruf, maarufu kama Daruwesh Rocket (Kusali Nnareke) amefariki dunia usiku wa kuamkia Januari 20,2026 akiwa na umri wa miaka 97, Kifo chake kimetokea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Marehemu Daruwesh Rocket alizaliwa mwaka 1928AD katika eneo la Momburu, mkoani Mtwara Kusini.
Alijulikana sana katika jamii kwa misimamo yake ya kidini na maisha ya ibada, huku jina la “Rocket” likiwa ni utani uliotokana na simulizi zilizodai kuwa hakuwa akitumia usafiri wa ndege kwenda Maka kuhiji, madai aliyokuwa akiyakana.
Katika ujana wake, marehemu aliwahi kulitumikia Taifa kama Askari Polisi wa Tanganyika.
Akiwa kazini mkoani Arusha, alikutana na Sheikh wa Kisufi wa Tariqatul Qadiriyyah, maarufu kama Daruwesh Mti Mkavu, mwenye asili ya Yemen, aliyefahamika kwa kueneza dini, maadili na ucha-Mungu.
Mwaka 1966, katika kipindi cha uongozi wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Daruwesh Rocket aliamua kuacha kazi ya uaskari na kujikita kikamilifu katika masuala ya dini.
Alipokea ijaza ya Tariqatul Qadiriyyah kutoka kwa Sheikh Daruwesh Mti Mkavu na baadaye kuithibitisha kwa Sheikh wake Sayyid Swaleh Izzudin wa Moshi, ambako alikabidhiwa bendera ya Udaruwesh kwa ajili ya kuendeleza kazi za dawa na Twariqa.
Katika maisha yake, marehemu Daruwesh Rocket atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kueneza mafundisho ya dini ya Kiislamu na maadili mema katika jamii.
Viongozi wa dini, wanafunzi wake na waumini wameendelea kutoa salamu za pole kwa familia, ndugu na jamaa kufuatia msiba huo.
