Serikali yataja mafanikio ya siku 100 za Rais Dkt.Samia, Bandari ya Dar es Salaam yaongeza ufanisi na mapato

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan imetaja mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha siku 100 za uongozi wake, hususan katika maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, ongezeko la mapato ya Serikali na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 20,2025 katika Bandari ya Dar es Salaam jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali,Bw.Gerson Msigwa amesema,Serikali imefanya maboresho makubwa katika bandari hiyo ambayo ni lango kuu la usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Msemaji Mkuu wa Serikali amebainisha kuwa, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Serikali imeendelea kuimarisha bandari ili kuongeza ushindani wa kikanda na kimataifa, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma kwa nchi jirani zinazotumia bandari za Tanzania.

Kwa mujibu wa Msigwa, katika mwaka wa fedha 2024/2025 bandari za Tanzania zilihudumia shehena kubwa kutoka nchi jirani zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Rwanda, Burundi, Malawi, Uganda na Zimbabwe, jambo linaloonesha imani kubwa ya kikanda kwa bandari za Tanzania.

"Mathalani katika kipindi cha mwaka 2024/25, bandari zetu za Tanzania zimehudumia nchi jirani zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo shehena ya tani 5, 995,293, Zambia shehena ya tani 3, 510,7062,Burundi shehena ya tani 425,774.

"Rwanda shehena ya tani 1,724,370,Malawi shehena ya tani 675,200,Uganda shehena ya tani 185,625, Zimbabwe shehena ya tani 61,306 na nyingine shehena 38,512."

Amefafanua kuwa,TPA ilisaini mikataba ya upangishaji na uendeshaji na kampuni za kimataifa za DP World MEA FZE na Adani International Ports Holdings Pte Limited, ambazo zilianzisha kampuni nchini Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, zikiwemo DP World Dar es Salaam Limited na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL).

Hadi kufikia Juni 2025, DP World ilikuwa imewekeza takribani shilingi bilioni 214.2 katika ununuzi wa mitambo ya kisasa, uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA,ukarabati wa karakana na upanuzi wa maeneo ya kuhifadhi shehena.

Kwa upande wake, TEAGTL imewekeza shilingi bilioni 410.4 katika ukarabati wa miundombinu ya gati namba 8 hadi 11, ununuzi wa mitambo mipya na usimikaji wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA.

Msigwa amesema,uwekezaji huo umeongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, ambapo shehena iliyohudumiwa iliongezeka hadi tani milioni 27.7 katika mwaka wa fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Aidha, katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026, bandari ilihudumia tani milioni 16.7, ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Msemaji Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa, muda wa kuhudumia meli za makasha umepungua kutoka wastani wa siku 30 hadi siku sita pekee, hatua iliyopunguza gharama za biashara na kuongeza ufanisi wa bandari.

Katika upande wa ajira, amesema uwekezaji huo umewezesha ajira za moja kwa moja 764 hadi kufikia Juni 2025, huku maelfu ya ajira zisizo za moja kwa moja zikiendelea kuwanufaisha Watanzania kupitia shughuli za usafirishaji, forodha na huduma nyingine.

Pia, amesema Serikali imenufaika kwa kuongezeka kwa mapato, ambapo mapato ya kodi ya forodha yalifikia shilingi trilioni 12.33 katika mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Vilevile, gharama za uendeshaji wa TPA zimepungua kwa wastani wa asilimia 57, na kuongeza uwiano wa faida kutoka asilimia 66 hadi 78.

Msigwa amesema, mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga uchumi shindani, kuboresha huduma kwa wananchi na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Kusini.

“Ni mapinduzi makubwa sana ndugu zangu Watanzania, na tuachane na maneno kuwa bandari imeuzwa lahasha, bandari haijauzwa haya ni maono ya Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan kuleta mapinduzi katika bandari zetu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here