DCEA yakamata tani 9 za dawa za kulevya,Mkenya muuza chai adakwa Sinza C

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kupitia operesheni kabambe zilizofanyika mwishoni mwa mwezi Desemba,2025 imefanikiwa kukamata kilo 9,689.833 za dawa za kulevya, pikipiki 11 na magari matatu.
Hayo yamebainishwa leo Januari 8,2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, katika operesheni iliyofanyika Sinza C katika Mtaa wa Bustani nyumba namba 16, Jefferson Kilonzo Mwende mwenye umri wa miaka 35 na raia wa Kenya alikamatwa akiwa na gramu 131.88 za hereoin.

"Mtuhumiwa huyo aliyeishi Tanzania tangu mwaka 2023, alitumia biashara ya kuuza chai kuficha biashara ya dawa za kulevya anayoifanya."

Pia, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, katika Mtaa wa Wailes uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam mamlaka hiyo ilikamata pakti 20 za skanka zenye uzito wa kilogramu 20.03 zikiwa zimefichwa ndani ya balo la mitumba na kufichwa kwenye basi aina ya Scania.

Basi hilo lenye usajili wa nchi ya Msumbiji namba AAM 297 CA ni mali ya Kampuni ya King Masai Tours, ambapo huwa linafanya safari zake kati ya Nampula nchini Msumbiji na Tanzania.

"Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Amasha Idd Mrisho miaka 40, ambaye ni mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam na Seleman Juma Ally miaka 32 raia wa Msumbiji."

Mbali na hayo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa, eneo la Kinyerezi katika Mtaa wa Majoka wilayani Ilala jijini Dar es Salaam walikamatwa watuhumiwa Erick Ernest Ndagwa miaka 32, Paul Blass Henry miaka 34 na Tido Emmanuel Mkude miaka 35 wakiwa na bangi kilo 193.66 zikisafirishwa kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.

Aidha,Kamishna Jenerali Lyimo amesema, kufuatia ukaguzi uliofanyika kwenye kampuni za usafirishaji wa mizigo jijini Dar es Salaam walikamata pakiti 20 za dawa z kulevya ainaya mirungi zenye uzito wa kilogramu 9.54.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema,dawa hizo za kulevya zilikamatwa zikiwa zimefungwa kama majani ya mwarobaini yaliyokaushwa ambapo zilikuwa zikisafirishwa kutoka Kenya kwenda Australia.

Ameongeza kuwa, kupitia operesheni hizo mikoa ya Shinyanga, Mwanza,Morogoro, Tanga,Lindi, Kilimanjaro, Njombe, Kigoma na Arusha zilikamatwa dawa za kulevya aina ya heroin gramu 37.34, skanka kilogramu 1.015, bangi kilogramu 7,969.98 na mirungi kilogramu 1,363.701 na kutekeleza ekari 14 za mashamba ya bangi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here