Kitulo Garden Marathon zazinduliwa rasmi

NJOMBE-Mbio, za Kitulo Garden Marathon, zimezinduliwa rasmi mkoani Njombe na Afisa Utamaduni wa Michezo wa Mkoa wa Njombe, Flavian Kitago akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mheshimiwa Anthony Mtaka ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo.
Mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Mei 2, 2026 katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, zimetajwa kuwa ni moja ya mbio za kipekee nchini, zikielezwa kufanyika katika uwanda wa juu kuliko mbio zote nchini, hali ambayo itawapa washiriki wa mbio hizo utofauti wa kimazingira na hali ya hewa ya kiutofauti.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio hizo, Kitago alieleza kuwa, uongozi wa Mkoa wa Njombe umefurahishwa na kuanzishwa kwa mbio hizo huku akisema kuwa itakuwa chachu ya maendeleo mkoani Njombe na hamasa ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo.

Pia alisema, hizo ni mbio za kwanza za Marathon kufanyika katika Mkoa wa Njombe, hivyo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wadau wote wa maendeleo mkoani Njombe na kote nchini kutumia fursa hiyo ya Marathon kujitangaza.
Ameeleza kuwa,uongozi wa mkoa utashirikiana kwa karibu na kamati ya mandalizi ya Kitulo Garden Marathon na awewakaribisha wageni wote kutoka pande zote za nchi na nje ya nchi kushiriki kwa wingi kwa kuhakikisha usalama wao wakati wa mbio hizo.

Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, Harry Gazi ametumia fursa hiyo kuelezea zaidi upekee wa hifadhi hiyo na umuhimu wa mbio hizo kufanyika Kitulo.

Gazi ameleeza kuwa Hifadhi ya Taifa ya Kitulo hutambulika kimataifa kama hifadhi ya Upendo, ambapo mwaka 2025 imeshinda tuzo ya Afrika kama kituo bora cha fungate (Africa's Best Honeymoon Destination), huku ikiingizwa katika kinyang'anyiro hicho hicho katika mashindano ya kidunia.

"Napenda kutumia fursa hii kuwakaribisha wageni kutoka pande zote za nchi kuja kutembelea hifadhi ya kitulo, na pia kuitumia Marathon hii kama njia yao mojawapo ya kufika na kufurahia urithi huu wa dunia wa kipekee wa hifadhi hii,"amesema Gazi.
Aidha, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Makete, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NMB Makete, Elinkaila Nashokigwa, ameeleza kuwa Benki ya NMB inaona fahari kubwa kuwa mdhamini mkuu wa mbio hii kwani ni mbio inayoenda kufungua fursa na kuwezesha huduma za jamii kitu ambacho kinaenda sambamba kabisa na sera za Benki ya NMB.

Naye Adam Akaro ambaye alimuwakilisha meneja wa CRDB Bank Tawi la Ikonda, Makete alieza kuwa CRDB Bank imefurahi kuwa miongoni mwa wadhamini wakuu wa mbio hii ya Kitulo Garden Marathon, huku akieleza kuwa CRDB Bank imedhamiria kutanua huduma zake wilayani Makete na udhamini wa CRDB Bank katika mbio hii unaiwezesha kufikisha huduma zake kwa jamii na kugusa maisha ya wengi wilayani Makete.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoani Njombe, Tegemea Mbogela alipongeza juhudi zote zinazofanyika kwa ushirikiano mkubwa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Uongozi na Wilaya ya Makete na Uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Kitulo katika kufanikisha maandalizi ya mbio hizi, huku akiwasihi wanariadha na wapenda michezo kutoka kote nchini kushiriki kikamilifu katika mbio hii ambayo itaweka historia ya kipekee kwao.

Akizunguza kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya Kitulo Garden Marathon, Monny Luvanda, ametumia fursa hiyo kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka na uongozi wake wa mkoa kwa kuipa kamati ushirikiano wa karibu kabisa kuhamikisha kuwa mbio hizo zinafanikiwa na kuandaliwa katika viwango vya kimataifa.
Aidha aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Makete, Uongozi wa Hifadhi ya Kitulo na Uongozi wa Chama cha Riadha Mkoa wa Njombe kwa ushirikiano wao mkubwa na miongozo muhimu wanayoipatika kamati ya maandalizi.

Monny amesema mbio hizo zinalenga kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha na kukuza utalii nchini ambazo alizianzisha kupitia program ya Royal Tour.

Pia ameongeza kuwa, mbio hizo zinaelenga kuigusa jamii ambapo sehemu ya mapato yake yameelezwa kuchagia huduma za elimu na afya katika jamii huku akisema kuwa, mbio hizo ni Full Marathon ambayo itajumuisha kilometa 42, kilometa 21.5, kilometa 10 na kilometa 5 huku zikitanguliwa na mbio za hiari za baiskeli (Cycling Fun Race) itayofanyika siku moja kabla yaani tarehe Mosi Mei, 2026 na waendesha baiskeli kujumuika na washiriki wa Marathon eneo la Kitulo Campsite mnamo Mei 2.

Ada ya ushiriki imeelekezwa kuwa shilingi 40,000 ambayo utaweza kujisajili huku wageni kutoka nchi za nje wakilipa ada ya dola za kimarekani 40, kiwango ambacho kitamwezesha mshiriki kujipatia Marathon Kit, Medali, namba ya BIB pamoja kugharamia gharama za kuingia hifadhini. Washiriki wanaweza kulipia ada zao za ushiriki muda wowote kuanzia sasa kwa kupitia aidha akaunti za benki ikiwamo CRDB Bank akaunti nambari 10180580827-KITULO GARDEN MARATHON.

NMB akaunti nambari 20310135782 KITULO GARDEN MARATHON, au kwa LIPA NAMBA YA MIX BY YAS 11946572 yenye jina KITULO GARDEN MARATHONS. Pia, washiriki na wadau wote wanaweza kujipatia taarifa zaidi kupitia tovuti maalum ya mbio hizi ya www.kitulogardenmarathon.com au kupitia mitandao ya kijamii kwa jina la Kitulo Garden Marathon.

Sambamba na hayo, uzinduzi huo ulibarikiwa kwa maombi yaliyoongozwa na Baba Askofu Stephen Nguvila wa KKKT Dayosisi ya Kusini Magharibi, ambaye aliambatana na Msadizi wa Askofu Mch. Christon Ngogo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here