KATAVI-Kwa mujibu wa wataalam wa kiafya imeelezwa kuwa, kumwachisha mtoto kunyonya kabla ya muda wa angalau miezi 6 na kuendelea hadi miaka miwili ni unyanyasaji dhidi ya mtoto kwani huathiri afya ya mtoto kwakuwa maziwa ya mama yana kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Mkaguzi wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto, Makao Makuu ya Polisi Dodoma, INSP Wilfred Willa ameyasema hayo Januari 21, 2026 mkoani Katavi alipokuwa akitoa mada kwa askari wa kike mkoani humo.
Ameongeza kuwa, mama anapomwachisha mapema mtoto kunyonya maziwa, kinga hupungua na anaweza kuugua mara kwa mara na kuathiri ukuaji wa akili na kimwili.
Amesema, maziwa ya mama yana virutubisho muhimu kwa ukuaji wa ubongo hivyo kuachishwa mapema kunaweza kuchangia udumavu au utapiamlo.
Aidha, amesisitiza kuwa kumwachisha mapema huathiri pia afya ya kihisia kwani kunyonya humpa mtoto faraja, usalama na uhusiano wa karibu na mama.
Aliwasisitiza kuwapa haki ya kunyonya kwa kuwa mtoto hana uwezo wa kujitetea au kuelewa kwa nini ananyimwa ambapo uamuzi wa mzazi usiozingatia maslahi ya mtoto ni ukandamizaji na unyanyasaji wa mtoto.Hata hivyo, aliezea kuwa kumuachisha kunyonya ni sehemu ya UHALIFU isipokua tu kuna hali chache za kiafya (kwa mama au mtoto) zinazoweza kulazimisha kuachisha mapema na hapo hufanyika kwa ushauri wa mtaalamu wa afya si kwa hiari au sababu zingine.
Mkaguzi Willa, aliwataka askari hao wa kike kutokua sehemu ya kuwaachisha watoto maziwa ya mama kwa visingizio vya kikazi kwa kuwa upo utaratibu wa kikazi wa kuwahudumia watoto wachanga.





