Mwelekeo chanya wa Uchumi waipa Tanzania matumaini mapya

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imebainisha kuwa, uchumi wa Tanzania Bara uliendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha ya takriban asilimia 5.9 mwaka 2025, ikilinganishwa na makadirio ya ukuaji wa asilimia 6.
Gavana wa BoT na Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba ameyasema hayo leo Januari 8,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na viongozi wa benki, taasisi za fedha pamoja na waandishi wa habari akitangaza Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa Robo Mwaka ya Kwanza 2026.

Katika mkutano huo, Gavana Tutuba ametangaza kuwa,Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate-CBR) cha asilimia 5.75 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026, kiwango ambacho kilitumika pia katika robo ya nne ya mwaka 2025.

Aidha, amesema ukuaji huu wa uchumi ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, madini na ujenzi.

Kwa upande wa Zanzibar,Gavana Tutuba amesema,ukuaji wa uchumi wa mwaka 2026 unakadiriwa kufikia asilimia 6.8, ukichangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, utalii na uzalishaji viwandani.

Vilevile, amesema,mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa wastani wa asilimia 20.3 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, Gavana Tutuba amesema,uchumi wa Tanzania Bara unatarajiwa kukua kwa asilimia 6, na uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2.

Pia, Gavana Tutuba amesema, mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu, ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 kama ilivyokuwa imepangwa.

Katika robo ya nne ya mwaka 2025, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa wa wastani wa asilimia 3.5, na kwa upande wa Zanzibar ulikuwa asilimia 3.4.

"Mwenendo huu mzuri ulitokana na utekelezaji madhubuti wa sera ya fedha, na mazingira mazuri ya kiuchumi duniani ambayo yalipunguza ongezeko la mfumuko wa bei kutoka nje ya nchi.

"Kamati inatarajia kuwa mfumuko wa bei utaendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 kwa robo hii."

Wakati huo huo, Gavana Tutuba amesema, sekta ya benki imeendelea kuwa imara, ikiwa na ukwasi wa kutosha kuwezesha utoaji wa
mikopo, pamoja na mtaji wa kutosha kuhimili misukosuko ya kiuchumi.

Aidha, vihatarishi katika utoaji wa mikopo vimeendelea kupungua ambapo uwiano wa mikopo chechefu (NPLs) ulipungua na kufikia asilimia 3.1, chini ya ukomo unaovumilika wa asilimia 5.

Gavana Tutuba anewapongeza wadau wa sekta ya fedha kwa jitihada zao zilizopelekea kupungua kwa uwiano wa mikopo chechefu hadi kufikia asilimia hiyo na kiwango kilicho chini ya ukomo unaovumilika.

Mifumo ya malipo imeendelea kuwa thabiti, ikifanya kazi kwa ufanisi katika maeneo ya mijini na vijijini.

"Sekta ya nje imeendelea kuimarika, ambapo nakisi ya urari wa malipo ya kawaida inakadiriwa kupungua hadi asilimia 2.2 ya Pato la Taifa (GDP) kwa mwaka 2025, ikiwa ni kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

"Mwenendo huu mzuri ulichangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya madini hususan dhahabu, mazao ya kilimo, kuimarika kwa shughuli za utalii na usafirishaji, pamoja na kushuka kwa bei za mafuta ghafi duniani."

Kwa upande wa Zanzibar, Gavana Tutuba amesema,sekta ya nje imeendelea kuwa na ziada katika urari wa malipo ya kawaida, ikichangiwa zaidi na mapato yatokanayo na shughuli za utalii.

Mbali na hayo, Gavana Tutuba amesema, ukwasi wa fedha za kigeni ulikuwa wa kutosha katika robo ya nne ya 2025, kutokana na ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya korosho, dhahabu na shughuli za utalii.

Thamani ya shilingi iliendelea kuwa tulivu dhidi ya sarafu nyingine, huku ikiongezeka thamani kwa takriban asilimia 0.8, mwishoni wa robo ya nne ya 2025.

Gavana Tutuba amesema, akiba ya fedha za kigeni ilifikia zaidi ya dola bilioni6.3, kiasi kinachoweza kufanya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takribani miezi 4.9, ikiwa ni juu ya lengo la angalau miezi 4.

"Akiba hii inatarajiwa kuendelea kuwa ya kutosha katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, sambamba na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi na kupungua kwa bei za mafuta."

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa sera ya bajeti umeendelea kuwa wa kuridhisha kwa Tanzania Bara na Zanzibar, huku makusanyo ya kodi yakiendelea kuongezeka.

Kuhusu Deni la Serikali, Gavana Tutuba amesema, liliendelea kuwa himilivu, ndani ya viwango vinavyokubalika kimataifa.

"Tathmini ya uhimilivu wa deni kwa mwaka
2024/25 inaonesha kuwa uwiano wa deni la umma kwa Pato la Taifa (kwa thamani ya sasa)
ulipungua hadi asilimia 40.6, kutoka asilimia 41.1 mwaka 2023/24, ikiwa chini ya ukomo
unaokubalika kimataifa wa asilimia 55."

Gavana Tutuba amewaeleza wadau hao kuwa, Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia kukutana tena Aprili 2,2026 na tangazo la Riba ya Benki Kuu kwa robo ya pili litafanyika Aprili 3,2026.

Ikumbukwe kuwa, uamuzi huo wa kubakiza CBR kama ilivyokuwa katika robo ya nne ya mwaka 2025, Gavana Tutuba amesema, utasaidia kuendelea kuchagiza ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini na kuwezesha ukuaji wa uchumi kuwa wa kuridhisha.

Kwa kuzingatia uamuzi huu, Benki Kuu itatekeleza sera ya fedha kwa kuhakikisha riba ya mikopo ya siku 7 baina ya benki (7‑day interbank rate) inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here